Dar es Salaam. Siku moja baada ya Frederick Sumaye kutangaza kung’oka Chadema na kusema atakuwa tayari kushirikiana na chama chochote, mwenyekitin wa NCCR-Mageruzi amemtaka waziri huyo mkuu mstaafu kusimamia maneno yake.
James Mbatia pia amesema Sumaye anapaswa kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Sumaye alitangaza kuhitimisha safari yake ya miaka minne ndani ya Chadema baada ya kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani Novemba 2015 akitokea CCM. Juzi alisema ameamua kuachana na Chadema, lakini hatajiunga na chama chochote cha siasa.
Sumaye alitumia mkutano huo kuelekeza shutuma kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema wanaomuunga mkono ndio waliosababisha aanguke katika uchaguzi wa Kanda ya Pwani pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu.
“Nipo huru kutumika na cha-ma chochote ikiwa ni pamoja na Chadema kwa kutoa ushauri na kadhalika,” alisema Sumaye.
Kutokana na uamuzi huo wa Sumaye baadhi ya wafuatiliaji wa siasa nchini wanaamini anaweza kuwa yuko njiani kurudi CCM kama wengine waliotoka chama hicho mwaka 2015.
Wakati huo, Sumaye alitangaza kujiunga na upinzani Agosti bila ya kutaja chama hadi Uchaguzi Mkuu ulipomalizika na mwezi Novemba ndipo alipojiunga na Chadema na kukabidhiwa kadi Desemba.
Lakini Mbatia anaona kwa sasa Sumaye, mwenye miaka 59, abakie Chadema kwa kuwa umri wake haumruhusu kwenda kwingine.
“Sumaye ni moja ya watu muhimu kwa taifa kwa kuwa ana uthubutu na hii ni sifa yake na ndiyo maana anasema hawezi kutoka katika siasa ila atabaki kuwa mshauri, nampongeza,” alisema Mbatia.
“Namheshimu na namshauri asiende chama chochote cha siasa. Umri wake unatosha, yeye abaki juu ya vyama. Kunapotokea tatizo linahitaji maridhiano basi yeye atabeba dhamana ya taifa letu,” alisema.
Mbatia alisema Sumaye alipofikia, apumzike na kutumikia wananchi kwa maslahi ya taifa na si kuangalia maslahi binafsi.
“Mimi (Mbatia) ni mtaalamu wa majanga, sitaki nimtabirie mabaya. Ili aheshimike ni bora asimamie kauli yake,” aliongeza Mbatia.
“Tunahitaji wengine waige mfano wake. Tuweke maslahi ya taifa mbele. Sisi tupo tayari.”
Licha ya kutotangaza kujiunga na chama chochote mwaka 2015, Sumaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji waliokuwa wakivutia wafuasi wa upinzani na hivyo kujijengea umaarufu zaidi.
Hadi sasa, Sumaye ndiye waziri mkuu pekee ambaye ameshikilia nafasi hiyo kwa vipindi viwili kamili vya miaka mitano kila kimoja baada ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kumuamini.
Lakini heshima hiyo aliyoijenga kwa upinzani mwaka 2015, haikufua dafu kwa wapigakura wa Kanda ya Pwani ambako aligombea peke yake uenyekiti na kujikuta akipigiwa kura 48 za kumkataa huku za kumkubali zikiwa 28 tu.
Naye mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe anashangaa sababu za Sumaye, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kanda hiyo na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, kuchukua uamuzi huo.
“Sumaye alikuwa na nafasi kubwa. Ametoka Chadema na sijajua sababu hasa. Sijui ni hasira au mambo aliyoyataka akiwa Chadema hayakuwa,” alisema.
Rungwe, ambaye aligombea urais mwaka 2015, alisema watakubali ushauri wake kama atakuwa tayari.
Alipoulizwa haoni kama Sumaye yuko njiani kurejea CCM, Rungwe alisema: “Mimi sifahamu anaelekea wapi.”
Kuhusu pengo la Sumaye ndani ya Chadema, Rungwe alisema: “Chadema kidogo kutakuwa hakuko sawa. Mtu maarufu kaondoka na karibu watu wazito wote wameondoka.”
Naye Katibu mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman alisema, “Tukikaa katika vikao na kuona kuna haja ya kushirikiana naye tutafanya hivyo na ikiwa hatutaona tutaamua.”
Ushauri mwingine ulitolewa na kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alipokea kwa mikono miwili uamuzi wa Sumaye kuwa tayari kushirikiana na vyama vyote.
“Chama (ACT-Wazalendo) hakitasita kumtumia Sumaye kutokana na uzoefu wake kwenye siasa,” alisema Zitto.
“Sisi tukiwa na lolote la kuomba ushauri wa Sumaye hatutasita kumwomba ushauri. Viongozi hawa wana maarifa mengi, uzoefu mwingi na mstaafu mwingine yeyote kama kuna jambo anaweza kusaidia tutaomba.”