Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lwakatare aanika kiini kustaafu kwake

LWAKATARE.webp Lwakatare aanika kiini kustaafu kwake

Wed, 10 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Asema uamuzi anao miaka mitatu *Umebeba baraka zote za wazee *Ajibu tuhuma kuihujumu CUF Tunduru

JANA katika sehemu ya pili ya mazungumzo haya ya faragha na Nipashe, mwanasiasa mwandamizi na Mbunge wa Bukoba Mjini anayestaafu, Wilfred Lwakatare, alikumbusha alivyochuana na Balozi Khamis Kagasheki kuwania ubunge mwaka 2005 na kushindwa kwa tofauti ya kura 148.

Vilevile, Kiongozi huyo wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alibainisha kilichomkimbiza Chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Leo, katika sehemu ya tatu ya mazungumzo haya, Lwakatare anafafanua kuhusu tuhuma za kutaka kutumiwa na CCM ili kuihujumu CUF katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Tunduru.

Mbunge huyo anaeleza kushtushwa na taarifa hizo za yeye kutaka kukihujumu chama chake katika kipindi ambacho alikuwa na wadhifa mkubwa ndani ya chama.

Pia, Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani wa CUF anafunguka mipango yake baada ya kuamua kustaafu ubunge mwezi huu pamoja na kilichomsukuma kuchukua uamuzi huo. Fuatilia maelezo yake: --- SWALI: Katika mchuano mzito wa uchaguzi mdogo wa Tunduru, ukiwa mtu muhimu wa chama chako dhidi ya Mtutura wa CCM, inaelezwa ulikuwa na mpango wa kuingia mkataba na mwanaCCM 'senior' Tunduru kupeleka gari lako akalisimamie kibiashara huko. Ikoje hii? Je, dokezo hilo halikuletea tabu kisiasa?

LWAKATARE: Wakati wa uchaguzi mdogo Tunduru ambapo chama changu wakati huo (CUF) kilimsimamisha marehemu Rajab Mazee, kijana huyu alikuwa shupavu na mwanamageuzi makini kindakindaki.

Nilishiriki mwanzo-mwisho kama kiongozi wa ngazi ya kitaifa ndani ya Chama cha CUF katika uchaguzi huo ambao ni kweli ulikuwa mzito. CUF iliibuka mshindi wa pili nyuma ya CCM na Chadema wakawa washindi wa tatu.

Hii habari ya kuwa mimi nilikuwa na 'plan' (mpango) ya kuingia mkataba na mwanaCCM ‘senior’ Tunduru kupeleka gari langu Tunduru alisimamie kibiashara, ni habari mpya kwangu, ni 'surprise'.

Sikumbuki kabisa kama niliwahi kuingia wala kujaribu kufikiria kufanya 'deal' kama hiyo. Huko ulikopata ubuyu huo ni vyema ukaparejea tena wakupe ufafanuzi wa kutosha na ikibidi na vielelezo ili suala hili uende nalo vizuri.

SWALI: Ndani ya siku chache zijazo wewe haupo tena bungeni, utakuwa mbunge mstaafu. Ni siasa kwa heri au ubunge tu? Tueleze kwa kina maana maisha lazima yaendelee.

LWAKATARE: Kwa walionisikiliza vizuri juu ya kustaafu kwangu kugombea ubunge, ni kwamba uamuzi huu niliufanya miaka mitatu nyuma kwa kuanza kuwataarifu wadau wanaonihusu juu ya masuala yangu ya kisiasa.

Baadhi haikuwa kazi nyepesi kuwashawishi. Wengi walikuwa na usemi kwamba bado umri unaruhusu, miaka 58! Na wengine kudai bado wapigakura wananihitaji na ninao ushawishi wa kutosha kuendelea kugombea na kupata ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini.

Nimegombea ubunge vipindi vyote tangu mwaka 1995. Nimeingia bungeni mara mbili kwa kura za kishindo na kwa kuwaangusha watu wazito.

Kugombea ubunge majukwaani inatosha. Wahaya wanasema "nalima ha harungi ainuka" (hata yule anayelima sehemu nzuri hupumzika).

Mimi ni mwanasiasa 'by profession' na kwa kusomea. Ninajivua vipi kazi yangu iliyonijaa mwili mzima nje ndani? Muhimu ni kwamba ninashiriki siasa zipi, kwa namna gani na kwa kiwango kipi na wapi na kina nani?

Nikiwa kama mstaafu, lazima nijipange vizuri. Na zaidi nisingependa kuingia siasa za kuninyima nafasi na muda wa kufanya shughuli zangu nilizojipanga kuniingizia kipato maana kama ulivyosema lazima maisha yaendelee.

Ninayo familia, mke na watoto, lazima nijipange nao kuyakabili maisha, lakini nisingependa kuyazika kuzimu maarifa lukuki niliyonayo nayo na nisiwamegee wengine wakati ningali hai.

Atakayependa kunifikia ili nimchotee sehemu ya maarifa niliyonayo katika masuala ya siasa endelevu za kuleta mabadiliko ya kuboresha maisha ya mwananchi na ulimwengu kwa kushirikiana, sitasita kufanya hivyo.

SWALI: Umekuwa ukiingia na kutoka kwenye ubunge. Huu ni utaratibu wa wananchi wa Bukoba au kuna siri ya siasa za kwenu?

LWAKATARE: Kila uchaguzi una joto lake kufuatana na aina ya uchaguzi, awamu ya utawala na namna 'inavyo-respond' na sheria, kanuni na taratibu zinazokuwa zimewekwa katika kipindi husika.

Mimi nilianza kushiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1994 nilipoamua kugombea uenyekiti wa mtaa, Mtaa wa Omukituli, Kata yangu ya nyumbani Kibeta, Bukoba mjini kwa tiketi ya CUF nikiwa mtumishi wa serikali.

Uchaguzi huo ulikuwa na vikwazo vikubwa ukichukulia maanani kuwa ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi serikali za mitaa baada ya sheria ya vyama vingi kupitishwa mwaka 1992.

Katika uchaguzi huo, uongozi wa mkoa na wilaya wa chama na serikali, ulilazimika kuja kumfanyia kampeni mgombea wa CCM katika mtaa wetu nilikogombea mimi.

Ninamshukuru Mungu na wakazi wenzangu wa Mtaa wa Omukituli walinichagua kwa kura nyingi mno. Washindani wangu waliondoka kwa aibu sana. Kiukweli iliwauma sana utafikiri ulikuwa uchaguzi wa kumpata mbunge.

Uzuri waliridhika na matokeo, wakayakubali na kuondoka kwenda kuugulia maumivu bila kuleta vurugu au kutumia nguvu. Na mimi nikaendelea na kazi bila kubughudhiwa.

Ukilinganisha hali hiyo na hali tunayoishuhudia hivi vipindi tunavyopita, ni mambo tofauti ya ajabu. Katika siasa, kuna mambo mengi sana.

Nikipata fursa na nafasi huko mbele, nitakuja siku moja kuwaelezeni na kuwapa 'facts' za uchaguzi uliofuata kwa miaka yote ya uchaguzi, kwani nilishiriki kwa vitendo, nikashinda na kushindwa.

Huko kushinda na kushindwa ndiyo hiyo uliyoiita kuingia bungeni. Tumekuwa na ushindani mkali wa kiasa kwa miaka mingi na hadi sasa bado hali hiyo ipo Bukoba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live