Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lwakatare: Kilichoniingiza siasa kero hizi, niliyoyakuta haya hapa

LWAKATARE.webp Lwakatare: Kilichoniingiza siasa kero hizi, niliyoyakuta haya hapa

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Aliusamehe uofisa, mishahara 3

SHAUKU iliyopitiliza kudai haki ndiyo ilimfanya Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, aitose ajira yake ya ofisa utumishi na utawala na kuilipa serikali mishahara mitatu ndani ya saa 24 ili ajiunge na siasa, Nipashe imeelezwa.

Katika mazungumzo maalum na Nipashe wiki iliyopita, Lwakatare (56), alisema ni uamuzi aliouchukua mwaka 1998, kipindi hicho akiitumikia Manispaa ya Bukoba baada ya kubaini anashindwa kuwa na uamuzi mkubwa dhidi ya mlolongo wa uonevu, madai yalipowasilishwa mezani kwake.

"Ni kweli mimi siasa niliziingia mwaka 1991 nikiwa mtumishi wa Halmashauri ya Mji Bukoba (wakati huo na kwa sasa manispaa)... Nilivyoingia kazini tangu mwanzo 1989, nilipenda utetezi wa haki kwa watendaji, kutetea na kuilinda haki za watumishi kazini.

"Uvunjifu na unyimaji haki watumishi, ni jambo lililokuwa likinikera wazi na mimi kulisemea. Japo nilikuwa ofisa utumishi, nafasi yangu haikuwa ya matawi ya juu yenye nguvu ya kuamua na kutenda.

"Hivyo, niliishia kwenye 'frustrations', jambo lililonipelekea mwaka 1998 kumwandikia mwajiri 'notice' ya saa 24 ya kuacha kazi na hivyo kumlipa pesa 'cash' (taslimu) mishahara yangu ya miezi mitatu kwa mujibu wa sheria za kazi.

Na hapo ndiyo ukawa mwanzo wa mimi kuingia kwenye siasa moja kwa moja na mwaka 2000 kufanikiwa kugombea ubunge Jimbo la Bukoba Mjini na kushinda kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF)," alisema.

Katika mazungumzo hayo ya faragha na Nipashe, Lwakatare pia aligusia hatua zilizochukuliwa dhidi yake na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kilichomsukuma kuamua kutowania tena ubunge. Ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo ya Nipashe na Mkurugenzi huyo wa zamani wa Idara ya Ulinzi na Usalama ya Chadema: --- SWALI: Ulikuwa ofisa wa Halmashauri ya Bukoba. Nini hasa kilikuingiza katika siasa za ubunge, tena upinzani?

LWAKATARE: "Ni kweli mimi siasa niliziingia mwaka 1991 nikiwa mtumishi wa Halmashauri ya Mji Bukoba (wakati huo na kwa sasa manispaa) na mwaka mmoja kabla ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa kisheria.

Historia yangu shuleni kuanzia elimu ya msingi, secondarI 'O' na 'A' Level na kisha JKT mwaka mmoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1985-1988, kwa wote niliobahatika kuwa nao, ni mashahidi wangu kuwa mimi ni mtu mwenye hulka ya kupenda kuhoji 'logically' mambo yoyote yanayojitokeza ndani ya taasisi husika yenye kuzua utata au kuibua hoja shindanishi.

Ni mtu niliyependa mijadala na nilisoma na kuyapenda masomo ya 'literature' (fasihi), fasihi simulizi na andishi. Ukweli nimekuwa mwathirika mkubwa wa 'carrier' yangu kimasomo.

Nilivyoingia kazini tangu mwanzo 1989, nilipenda utetezi wa haki kwa watendaji, kutetea na kulinda haki za watumishi kazini, huku nikiwa Ofisa Utumishi na Utawala.

Hali hiyo inipelekea kutunukiwa ufanyakazi bora mara mbili ndani ya kipindi changu cha miaka 13 ya utumishi serikalini na katika vituo mbalimbali. Hivyo, uvunjifu na unyimaji haki watumishi, ni jambo lililokuwa likinikera wazi na mimi kulisemea.

Japo nilikuwa Ofisa Utumishi, nafasi yangu haikuwa ya matawi ya juu yenye nguvu ya kuamua na kutenda. Hivyo niliishia kwenye 'frustrations', jambo lililonipelekea mwaka 1998 kumwandikia mwajiri 'notice' ya saa 24 ya kuacha kazi na hivyo kumlipa pesa ‘cash’ mwajiri mishahara yangu ya miezi mitatu kwa mujibu wa sheria za kazi.

Na hapo ndiyo ukawa mwanzo wa mimi kuingia kwenye siasa moja kwa moja na mwaka 2000 kufanikiwa kugombea ubunge Jimbo la Bukoba Mjini na kushinda kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).

SWALI: Ulionaje joto la siasa na nini siri ya ushindi wako?

LWAKATARE: Kila uchaguzi una joto lake kufuatana na aina ya uchaguzi, awamu ya utawala na namna 'inavyo-respond' na sheria, kanuni na taratibu zinazokuwa zimewekwa katika kipindi husika.

Mimi nilianza kushiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1994 nilipoamua kugombea uenyekiti wa mtaa -- Mtaa wa Omukituli, kata yangu ya nyumbani Kibeta, Bukoba mjini kwa tiketi ya CUF nikiwa mtumishi wa serikali.

Uchaguzi huo ulikuwa na vikwazo vikubwa ukichukulia maanani kuwa ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi serikali za mitaa baada ya sheria ya vyama vingi kupitishwa mwaka 1992.

Katika uchaguzi huo, uongozi wa mkoa na wilaya wa chama na serikali, ulilazimika kuja kumfanyia kampeni mgombea wa CCM katika mtaa wetu nilikogombea mimi.

Ninamshukuru Mungu na wakazi wenzangu wa Mtaa wa Omukituli walinichagua kwa kura nyingi mno. Washindani wangu waliondoka kwa aibu sana. Kiukweli iliwauma sana utafikiri ulikuwa uchaguzi wa kumpata mbunge.

Uzuri waliridhika na matokeo, wakayakubali na kuondoka kwenda kuugulia maumivu bila kuleta vurugu au kutumia nguvu. Na mimi nikaendelea na kazi bila kubughudhiwa.

Ukilinganisha hali hiyo na hali tunayoishuhudia hivi vipindi tunavyopita, ni mambo tofauti ya ajabu. Nikipata fursa na nafasi huko mbele, nitakuja siku moja kuwaelezeni na kuwapa 'facts' za uchaguzi uliofuata kwa miaka yote ya uchaguzi, kwani nilishiriki kwa vitendo, nikashinda na kushindwa.

*USIKOSE KESHO KUFUATILIA MFULULIZO WA MAZUNGUZO HAYA

Chanzo: www.tanzaniaweb.live