Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi: Nimepata kura za heshima, ujasiri

Lukuviii Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi amesema licha ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kura alizopata ni za heshima na ujasiri.

Lukuvi ni miongoni mwa wabunge walioangushwa katika kinyang’anyiro hicho, wakiwamo pia Jerry Silaa (Ukonga), Deodatus Mwanyika (Njombe), Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Mjini), Japhet Hasunga (Vwawa) na Abbas Tarimba (Kinondoni).

Pia, Waziri wa Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini nao walishindwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu juzi, alisema katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, hivyo anawashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kura walizompa.

“Utamaduni wa chaguzi ndani ya chama chetu mimi naujua una majibu mawili tu, kuna kushinda na kushindwa. Mimi kura zangu hazikutosha safari hii, lakini nimepata kura za heshima, hazikushinda kwa ile margin, maana nimekosa kura 11, lakini ni kura za heshima,” alisema.

Aliwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kumpigia kura za heshima na japo hazikutosha, anasema, “kwangu ni kura za ujasiri na heshima.”

Hata hivyo, anaendelea kubeba historia kubwa ya kuwa mbunge kwa muda mrefu kuliko wengine na utumishi mrefu serikalini.

Aliingia bungeni mwaka 1995 na kwa kipindi chote hicho amekuwa Mbunge kwa miaka 27.

Pia, ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini, akianzia Naibu Waziri na baadaye Waziri katika wizara tofauti.

Lukuvi ambaye kitaaluma ni mwalimu, alianza safari yake ya siasa katika Umoja wa Vijana wa CCM, akiwa katibu wa Wilaya za Masasi, Mtwara, Arusha na Dodoma.

Pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu na kamati ya utekelezaji ya Taifa ya UVCCM, kabla ya kuwa mkuu wa idara ya Oganaizesheni.

Nafasi nyingine alizoshika UVCCM ni pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye kuwa Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo kitaifa.

Mbali na UVCCM, amewahi pia kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya Wilaya, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, amewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu na Mjumbe wa Kamati ya Maadili Taifa.

Katika Serikali, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera mwaka 1994 na baada ya kushinda ubunge mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Kazi na Maendeleo ya Vijana, nafasi aliyoshika hadi mwaka 2000.

Mwaka 2000 hadi 2005, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa kwanza wa Dodoma na baadaye Dar es Salaam akiwa pia mbunge.

Baada ya uchaguzi wa 2010 alirejeshwa Ofisi ya Waziri Mkuu hadi mwaka 2014 na baada ya hapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, nafasi aliyoendelea nayo hadi Januari 2022 alipoenguliwa, hata hivyo bado anaendelea kuwa Mbunge.

Wakati Lukuvi akieleza hayo, Mmiliki wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka amewashukia watu wanaowabeza mastaa waliopigwa chini katika U-NEC.

Katika uchaguzi huo, miongoni mwa mastaa waliojitokeza kugombea mbali na Asha Baraka alikuwepo Haji Manara, mfanyabiashara Fred Ngajiro maarufu Vunja Bei, msanii wa filamu na muziki Zuwena Mohame ‘Shilole’ na msanii wa filamu, Halima Yahaya ‘Davina’ ambao wote hakuna aliyeshinda.

Jana, Asha akizungumza na Mwananchi alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi huo baadhi ya watu wamekuwa wakiwabeza mastaa walioshindwa na kuwapa majina ya ajabu, jambo ambalo si sawa.

“Hebu fikiria katika uchaguzi huo watu 2,001 walijitokeza kuwania na hata mchujo ulipofanyika na sisi majina yetu yalirudi na kwenda kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu. Mnajua kuwa kuna watu majina yao hata hayakurudi,” alisema.

Katika mchakato huo, zaidi ya wana CCM 2,000 walijitosa kuwania nafasi za U-NEC Tanzania Bara na Visiwani.

Chanzo: Mwananchi