Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lukuvi; Katiba ya CCM inanitaka kuitisha Mkutano Mkuu wa Jimbo

72853 Lukuvi+pic

Mon, 26 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kila aliyekuwa na dukuduku, hoja, pongezi au swali alipewa nafasi ya kumuuliza mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi kisha kupewa majibu ya papo kwa papo.

Kuna ambao changamoto zao zilitatuliwa na wakuu wa idara za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini wakati huo huo huku wengine wakitakiwa kusubiri utatuzi wake baadaye.

Ni nadra kwa mbunge au kiongozi mwingine wa kuchaguliwa kuacha uwanja huru kwa wananchi kuhoji utekelezaji wa ahadi alizotoa wakati anaomba kura ili apewe nafasi hiyo.

Hilo halikumsumbia Lukuvi ambaye alipata nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Isimani alioitisha ili awaeleze utekelezaji wa shughuli za maendeleo tangu mwaka 2015, alipoingia madarakani mpaka sasa.

Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi anasema aliitisha mkutano huo kikatiba kwa sababu anapaswa kuwaambia wananchi wake nini kimefanyika katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

“Natakiwa kuitisha mkutano huu mara moja katika kipindi cha miaka mitano hivyo nimeuitisha kikatiba, nachotaka kufanya ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, nimeandaa vitabu na nitagawa kwa kila balozi, ” anasema Lukuvi

Pia Soma

Mkutano Mkuu wa Jimbo ndio wenye mamlaka ya kupiga kura za maoni za kuwachagua wabunge na madiwani watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu au marudio kwenye jimbo husika.

Na huo ndio ambao humpa nafasi mbunge wa CCM kueleza nini amefanya tangu alipopewa kijiti cha kuongoza jimbo husika.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa Rose Tweve anasema licha ya majukumu mazito ya Lukuvi kwenye wizara yake, yupo sambamba na wananchi wake jambo linalopaswa kuigwa na wabunge wengine.

Moja ya kero iliyotatuliwa papo hapo kwenye mkutano huo ni malalamiko ya wananchi wa vijijini kutozwa zaidi ya Sh27,000 kwa ajili ya kuingiziwa umeme kwenye nyumba zao kinyume na tamko la Serikali.

Mkazi wa kijiji cha Mboliboli, Matrida Mkalangi alilalamika kushindwa kuingiza umeme kwenye nyumba yake akidai kuwa alitakiwa kulipa zaidi ya Sh300,000 fedha ambayo hakuwa nayo.

Kutokana na hilo, Waziri Lukuvi alimuinua Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ambaye naye, alimtaka Meneja wa Tanesco kutolea ufafanuzi kisha kuhakikisha nyumba ya Matrida na wengine wenye malalamiko kama hayo wanaingiziwa umeme kwa bei iliyotangazwa na Serikali.

Lukuvi anasema asilimia 99 ya vijiji vya jimbo hilo tayari vimeingiziwa umeme.

“Vijiji vilivyobaki ni Isaka, Mkwava na Mkubwani peke yake lakini kote umeme umefika, awamu ijayo itakuwa ni kusambaza kwenye vitongoji lakini kwa sasa kila kijiji kina umeme,” anasema Lukuvi.

Kazi nyingine alizofanya Isimani

Katika taarifa yake Lukuvi anasema jimbo hilo limetekeleza shughuli za maendeleo kupitia fedha za Serikali, Mfuko wa Jimbo na jitihada zake binafsi kama mbunge.

Anasema katika sekta ya kilimo mkakati wa jimbo hilo ni kuhakikisha mchele unaozalishwa Isimani unakobolewa na kuwekewa lebo yake ili ukifika mjini ujulikane umetoka huko.

“Maajabu ni kwamba mchele ukiwasili mjini wanadanganya kwamba umetoka Kyela wakati unalimwa Idodi na Pawaga, katika hili tumenunua mashine ya kukoboa na tayari yamejengwa maghala,” anasema Lukuvi.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu anasema wananchi wamefundishwa mbinu za kilimo bora na mpunga unaolimwa sasa ni ule unaotumia mbegu za kisasa.

Afya

Lukuvi anasema tangu mwaka 2015 huduma za afya kwenye jimbo hilo zimeimarishwa kwa kujengwa zahanati mpya, ukarabati wa vituo vya afya pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Anasema zahanati tisa kati ya 30 zilizo kwenye jimbo hilo zinaendelea kujengwa na zipo katika hatua mbalimbali.

“Upatikanaji wa vifaa pia umeimarika nami nilitoa vifaa tiba nyenye gharama ya Sh650 milioni nikipewa ufadhili na Wamarekani, hii imesaidia huboresha huduma kwa wananchi,” anasema Waziri Lukuvi.

Anataja zahanati mpya zinazoendelea kujengwa kuwa ni Makatapola, Mbweleli, Hollo, Mawindi, Kihorogota, Mikongwe, Kinywang’anga, Igingilanyi na Magozi.

Maji

Lukuvi anasema ujenzi wa mradi wa maji toka Izazi hadi Migori Mtera umekamilika kwa asilimia 95.

Anasema Sh1.3 bilioni zimeshalipwa ikiwa ni gharama za mradi husika na tayari wananchi wa eneo hilo wameanza kupata maji safi na salama.

Miradi mingine ya maji iliyokamilika ni mradi wa Izazi mpaka Mnadani, mradi wa maji toka Iruwasa kwenda Igingilanyi na Kising’a na mradi wa kufunga pampu za maji kwenye vijiji 19 jimbo hilo.

Maeneo mengine ni Ujenzi wa mradi wa maji Pawaga-Mlenge huku tenda ya mradi mkubwa wa maji wa Isimani ikitarajiwa kutangazwa wakati wowote mwaka huu na kwamba huo utakuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji Isimani.

Uchumi

Mbunge huyo wa Isimani anasema vikundi 222 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wamepatiwa mikopo ya kiuchumi na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa jambo lililosaidia kukuza maendeleo ya eneo hilo. Anasema tangu mwaka 2015 mpaka sasa Sh476.5 zimetolewa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi hivyo.

Elimu

“Kama ijulikanavyo elimu ni ufunguo wa maisha, jimbo hili limekuwa likijitahidi kuhakikisha kila mtoto anayetakiwa kwenda shule anaingia darasani,” anasema Lukuvi.

Anasema wamekuwa wakihamasisha wananchi kujitolea katika ujenzi wa miundombinu kama madarasa huku yeye akihakikisha vifaa muhimu vya ujenzi vinapatikana.

“Watu wa Isimani wamejitolea sana kujenga madarasa, nyumba za walimu, vyoo, mabweni, majengo ya utawala. Wanafanya haya tukishirikiana nami pamoja na Serikali,” anasema Lukuvi.

Udahiri wa wanafunzi wa jimbo hilo umeongezeka kutoka 4,124 mwaka 2015 mpaka kufikia 5,993 mwaka 2017 kwa sababu ya utolewaji wa elimu bila malipo.

Anasema Serikali imetumia Sh648.3 milioni kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo.

Jimbo hilo lina shule za msingi 69, sekondari tisa huku shule mbili za sekondari katika kijiji cha Izazi na Makifu zikiendelea kujengwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz