Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa ni uzalendo au mahaba ya chama?

45090 Uzalendo+pic Lowassa ni uzalendo au mahaba ya chama?

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanzania yetu, itajengwa na uzalendo wetu, itajengwa na “utaifa” wetu, itajengwa na mahaba na upendo wetu kwa nchi yetu. Tanzania yetu itajengwa na mshikamano wetu na roho ya kujitoa muhanga kulifia taifa letu. Kamwe Tanzania haitajengwa na mahaba na mapenzi ya vyama vya siasa.

Watanzania wengi hawako kwenye vyama vya siasa na kwa bahati mbaya vyama vya siasa vyote tulivyonavyo hadi leo hii, havijaweza kuonyesha pasi na shaka kwamba viko kulijenga taifa letu mbali na mahaba ya vyama vyao.

Mheshimiwa Edward Lowassa, alipojiengua CCM na kujiunga na Chadema, sisi wachambuzi na wazalendo wa taifa letu, tulifurahi na kufikiri kwamba sasa mheshimiwa Lowassa, anatambua kwamba taifa letu litajengwa na uzalendo wetu na wala si mahaba ya vyama vya siasa. Juzi, ameamua kututangazia kwamba tulimchukulia ndivyo sivyo. Yeye anaamini kwenye mahaba ya vyama vya siasa!

Ndiyo maana tunajiuliza juu yake. Anasukumwa na siasa, mahaba ya vyama vya siasa au moyoni mwake kuna uzalendo wa taifa letu? Je, ni shinikizo? Wengine wanasema tukio la mheshimiwa Lowassa, kurudi CCM ni la kisiasa tu, na sote tunajua kwamba siasa ni mchezo mchafu! Hakuna aliyetegemea kwamba Lowassa, anaweza kukaa meza moja na upinzani na hasa Chadema, wakaongea lugha moja na kushirikiana kutaka kuiondoa CCM madarakani.

Au kwamba Lowassa na Sumaye wanaweza kushirikiana kiasi ambacho tulishuhudia wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015.

Wanaomchukia Lowassa, wanasema ameugua ugonjwa wa kusahau. Eti hana kumbukumbu tena ya kujiengua CCM na kukimbilia upinzani! Kwamba inawezekana hata yale yote wanayoyasema juu yake, hayakumbuki wala kuyasikia! Kwamba ni mgonjwa kiasi yote yanayotendeka hana habari.

Ndo maana anakuwa kimya na harudishi tukano kwa tukano! Wengine wanasema badala ya kusema “peoples’s power” alikuwa akisema “CCM”, na akiwa Tanga, aliwaambia watu kwamba wakimchagua atakuwa “ rais mzuri wa Burundi”. Kwamba kuna wakati mwingine alisahau kwamba yeye yuko Tanzania, kichwani inaingia “Burundi”. Lakini huu ni uongo mtupu.

Tuliambiwa kwamba Lowassa, ni mgonjwa na hana uwezo kwa kufanya kampeni. Leo, tunaona anadunda, wengi waliosema ni mgonjwa, wametangulia tayari mbele haki. Maana yake ni kwamba huyu ni mzima na anazo kumbukumbu zote, kutojibu mapigo ilikuwa ni mbinu na mkakati wa kutimiza lengo lake na hatimaye kurudi nyumbani CCM. Na kweli, juzi amesema maneno machache sana kwamba amerudi nyumbani CCM, kana kwamba kuwa upinzani alikuwa nchi jirani ya Burundi!

Tuna weza kujituliza kwa msemo wa hakuna rafiki na adui wa kudumu katika siasa. Lakini, kwa mtu aliye makini ni lazima afikiri zaidi ya hapo. Taifa letu linapitia kipindi kigumu. Ni mara ya kwanza kitu kama hiki kutokea. Watu kuhama vyama vyao vya siasa bila mpangilio kwa lengo la kutafuta vyeo na madaraka.

Padre Privatus Karugendo

+255754633122

[email protected]



Chanzo: mwananchi.co.tz