Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa, mkewe wamdhamini JPM

Lowassa Lowassa, mkewe wamdhamini JPM

Thu, 25 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mke wake, Regina Lowassa, wameungana na mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kumdhamini mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Rais John Magufuli.

Rais Magufuli anatarajiwa kutetea nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu akiwa hajapata upinzani ndani ya chama chake mpaka sasa.

Hatua ya Rais Magufuli kutopata mpinzani ndani ya chama chake kunatokana na utaratibu uliowekwa ndani ya CCM wa kumwachia Rais aliyeko madarakani amalizie kipindi chake cha pili cha miaka mitano.

Jana, Lowassa na mamia ya wanachama wa chama hicho walikusanyika kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Monduli kutia saini zao kwa ajili ya kumdhamini mgombea huyo wa urais, ili kukidhi matakwa ya katiba ya chama hicho.

Katiba ya CCM inamtaka kila anayetaka kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, kudhaminiwa na wanachama 450 kwa mikoa minane ya Bara na miwili ya Zanzibar.

Lowassa ni mwanasiasa machachari ambaye baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Dk. Jakaya Kikwete, alihamia Chadema na kusimamishwa kuwania urais kwa tiketi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akiwa mgombea wa Ukawa, Lowassa atakumbukwa kwa namna alivyotia hamasa uchaguzi huo, akichuana vikali na aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Rais Magufuli na kufanikiwa kupata kura milioni 6,072,848 dhidi ya milioni 8.882,935 za mshindi.

Katika vuguvugu la uchaguzi huo wa mwaka 2015 ndani ya CCM, jina la Lowassa lilionekana kuwa maarufu kati ya wagombea wengine 42 waliojitokeza kukiomba chama chao kupeperusha bendera yake kwenye uchaguzi huo.

Na kwenye hatua za awali ambapo CCM ilimtaka kila mgombea kudhaminiwa na angalau wanachama 450, Lowassa alifikisha watu 700,000 waliokubali kumdhamini, ingawa jina lake lilikatwa katika hatua za mwanzo kabisa na kukosekana katika yale yaliyoingia hatua ya tano bora.

Katika mchakato huo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM walitoka hadharani na kutamka mbele ya waandishi wa habari kuwa hawakubaliani na uamuzi wa kumkata Lowassa.

Wajumbe wa CC, Adam Kimbisa, Dk. Emmanuel Nchimbi na Sophia Simba, aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT, walisema kuna njama zilifanyika na walisema waziwazi kwamba hawakubaliani na uamuzi huo wa CC.

NEC ilipokaa kupokea majina yaliyopitishwa na CC kwa ajili ya kupigiwa kura, baadhi ya wajumbe walisimama na kuimba kuwa wana imani na Lowassa wakati Mwenyekiti wa chama hicho wakati huo, Dk. Kikwete alipokuwa akiingia ukumbini.

Baada ya mchakato huo wa kumpata mgombea wa CCM, Lowassa aliamua kuhamia Chadema akifuatwa na kundi kubwa la wana CCM kukihama chama hicho wakiwamo waliokuwa na nyadhifa mbalimbali kama wabunge, wenyeviti wa mikoa na makatibu.

Machi Mosi, mwaka jana, Lowassa alitangaza kurejea CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli kwenye ofisi ndogo za chama hicho jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo mafupi aliyoyatoa mbele ya wafuasi wachache wa CCM walioshuhudia kurejea kwake siku hiyo, Lowassa alisema kwa kifupi "nimerejea nyumbani".

KILICHOMPAISHA

Kilichompaisha zaidi Lowassa katika hekaheka zake za kisiasa ni kambi yake ya urais iliyobatizwa jina la utani 'Boys Two Men' mwaka 1995.

Ni kambi iliyowahusisha Dk. Kikwete na Lowassa ambapo mwaka 1995 walikwenda Dodoma kwa ndege ya kukodi kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM.

Safari ya wawili hao ilianza kufifia baada ya jina la Lowassa kukatwa mapema na jina la Kikwete kufika kwenye mkutano mkuu uliofanyika Ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.

Matumaini ya Boys Two Men yalibaki kwa Kikwete lakini mkutano mkuu wa CCM uliohudhuriwa na Mwalimu Nyerere ulikatisha ndoto ya Kikwete baada ya Benjamin Mkapa kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 1995.

Wakati Kikwete anamalizia awamu yake ya pili, Lowassa alikuwa bado na imani ya ushirikiano wa Boys Two Men, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani jina lake lilikatwa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM na baadaye alilazimika kutimkia Chadema.

Lowassa aliyezaliwa Agosti 26, 1953 huko Monduli mkoani Arusha, aliteuliwa na Kikwete kuwa Waziri Mkuu hadi Februari 2008 alipojiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya Richmond.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live