Monduli. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amezindua kampeni za ubunge Jimbo la Monduli huku jina la Edward Lowassa likitawala kwenye mkutano huo.
Wakizungumza kwenye mkutano wa kumnadi mgombea wa CCM, Julius Kalanga zilizofanyika uwanja wa soko la Monduli, viongozi wengi wa CCM isipokuwa Mangula walikuwa wakilitaja jina la Lowassa wakati wakieleza sababu za aliyekuwa mbunge wa Chadema wa jimbo hilo kujiunga na CCM.
Viongozi hao walirejea kauli zao kuwa, Lowassa yupo njiani kurudi CCM na waliohama wamemtangulia tu.
Aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli na diwani wa Monduli Mjini, Isack Joseph ambaye hivi karibuni alijiuzulu udiwani na kujiunga na CCM, alisema kabla ya uamuzi huo alikwenda mara tatu kuonana na Lowassa.
Joseph alisema katika safari zake kwa Lowassa alimweleza kuwa ni vigumu kwao kama madiwani wa Monduli kuendeleza maendeleo aliyoyaacha kwani wapo upinzani.
Alidai kuwa Lowassa alimjibu kuwa muda wa wao kuondoka Chadema bado, wasubiri hadi mwaka 2019.
“Mimi ndiye nilikuwa rafiki wa karibu wa Lowassa hapa Monduli nilimwambia sisi kuendelea kuwa Chadema ni kuwaumiza wananchi, kwani hakuna msaada wowote kutoka Chadema,” alisema.
Alisema Chadema inapokea ruzuku zaidi ya Sh390 milioni kila mwezi, lakini imeshindwa hata kuajiri makatibu wa wilaya ama kujenga hata zahanati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo naye alisema Lowassa yupo njiani kurudi na kwamba wao wako tayari kumpokea.
Alisema Lowassa anawachezea wananchi wa Monduli kwani anajua kuwa yeye bado ni waziri mkuu mstaafu ambaye anatembelea gari la Serikali, analindwa na walinzi wa Serikali.
Alisema yeye kama mkuu wa mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, hivyo atawashangaa ambao watashangaa kumuona jukwaani akimnadi mgombea wa CCM.
Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare alisema anawataka wananchi wa Monduli kumchagua Kalanga na kuachana na propaganda.
Alisema kama Lowassa angekuwa anawatakia maendeleo wananchi wa Monduli angegombea yeye au mtoto wake, Fred Lowassa.
Aliwataka wakazi wa Monduli kutorejea makosa kuchagua upinzani, kwani sasa wanapaswa kuonyesha wanamuunga mkono Rais John Magufuli kutokana na kazi nzuri anayofanya.
Akizindua kampeni hizo, makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alisema kumekuwepo na maneno ambayo si sahihi kuwa taratibu za chama zinakiukwa kupitishwa wagombea bila kura za maoni.
“Hakuna taratibu zilizokiukwa kama kunakuwa na mgombea mmoja hakuna haja ya kura za maoni,” alisema.
Mangula alisema pia chama kinatazama mgombea ambaye anaungwa mkono na wengi na kueleza katika uchaguzi uliopita, Kalanga alipata kura 35,000 na kuwashinda wengine.
Mangula alieleza kuridhishwa na umati wa wanaCCM, waliojitokeza kwenye kampeni hizo na mapokezi makubwa waliyompa.
Alisema katika uchaguzi huo hawashindanishi ilani za uchaguzi kwani tayari ilani iliyopo ni ya CCM ambayo ndio mipango yake imepitishwa na wabunge.