Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa, Mgeja wasema Guninita alikuwa jasiri

17993 Pic+guninita TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja wamesema Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam John Guninita alikuwa ni mtu jasiri na mwaminifu enzi za uhai wake.

Wamesema hayo leo Septemba 18,2018 wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Gunininita zilizofanyika nyumbani kwake Tabata Kimanga, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Guninita alifariki dunia Septemba 13 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu akisumbuliwa na kwikwi na kiungulia lakini baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika na uvimbe tumboni.

Lowassa ambaye aliambatana na mkewe Regina, alisema atamkumbuka Guninita kwa mambo mengi, ikiwemo ujasiri wa kufanya uamuzi hasa pale ambapo hakubaliana na mambo kadhaa.

“Nilisononeka sana baada ya kupata taarifa za kifo cha Guninita. Alikuwa ni rafiki yangu ambaye tumeshirikiana kwenye vitu vingi, tumuombee kwa Mungu,” amesema Lowassa

Kwa upande wake, Mgeja alisema Guninita alikuwa ni kiongozi mwenye ujasiri na mwenye kusimamia kile alichokua akikiamini.

Amesema Guninita alikuwa hapindishi maneno, mtu wa kuunganisha watu na hakuwa na chuki pindi mnapotofautiana kwenye masuala mbalimbali.

“Huyu alikuwa kaka yangu kwenye siasa. Nitamkumbuka sana Guninita alikuwa ni mtu msikivu na asiyependa kulipiza kisasi pindi anapokosewa,” amesema Mgeja.

Kwa upande wake, mdogo wa marehemu Gerald Guninita alisema kifo cha kaka yake kimeacha pigo katika familia na ameacha watoto watano, wawili wa kike, watatu wa kiume na mjukuu mmoja.

Gerald alitumia nafasi hiyo, kumshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Lowassa, Mbunge wa Viti maalumu CCM, Mchungaji Getrude Lwakatare kwa ushirikiano wao wakati wa kumuuguza Guninita hadi alipofariki dunia.

“Kaka alianza kuugua Agosti mwaka huu na alilazwa Muhimbili. Tunawashukuru pia madaktari na waaguzi wa hospitali kwa ushirikiano wao,” amesema Gerald.

Shughuli za kutoa heshima za mwisho za mwili wa Guninita, zilianzia nyumbani Kimanga na kumalizikia katika Kanisa la Kristo Mchungaji Mwema lililopo jirani na kwake, kisha utasafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya maziko.

Akiendesha ibara ya kumuombea Guninita, Padri Gaudence Lyaruu amesema maisha ya duniani ni safari yenye milima na mabonde ambayo yana mwisho na ni vyema watu wakajiandaa.

“Dunia ni njia ya kuelekea sehemu ya kuanza maisha mapya. Tunachotambua ni kifo kipo, lakini hatujui nani anatangulia au atakufa lini ni vyema watu wakajiandaa kwa matendo mema.

“Kazi yetu kubwa leo ni kumwombea Guninita, Lakini tujiombee na sisi kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya baadaye,” alisema Padri Lyaruu.

Mamia ya wakazi wa Dar es Salaam, walihudhuria shughuli za kumuaga Guninita, wakiwemo kina Lowassa, Mgeja, Mchungaji Lwakatare na Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, Kate Kamba.

Chanzo: mwananchi.co.tz