Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa, Mbowe walivyobeba siri ya Kalanga, Waitara ndani ya Chadema

10043 Pic+mbowe TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Oktoba 2, 2015 aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa alimnadi mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Monduli, Julius Kalanga huku akieleza kuwa angezungumza na mgombea ubunge wa CCM, Namelok Sokoine kuona kama angekubali kupanda ‘basi’ la Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 kwenye mkutano wake wa kwanza Monduli uliofanyika Mto wa Mbu, Lowassa aliulizwa na wananchi kuhusu mustakabali wa Namelok ili wajue kama wamchague Kalanga au binti huyo wa waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine.

Akiwahutubia wananchi wa Mto wa Mbu katika Uwanja wa Barafu, Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20 alisema angekutana na Namelok siku hiyohiyo ili waelewane kwa kuwa asingependa kuvunja umoja wao wa muda mrefu.

“Kuhusu suala la ubunge nimekuwa mbunge kwa miaka 20, hivyo natakiwa nijue mbunge atakayefuata. Nitakubaliana na Namelock, akikataa kupanda basi hili basi,” alisema Lowassa huku baadhi ya vijana wakitaka kujua wamfanye nini Namelock.

Lowassa alisema anataka Monduli ibaki ileile yenye amani na utulivu na ambaye hataki kupanda kwenye basi lake ataachwa.

Wakati Lowassa akizungumzia suala la kujadiliana na Namelok, mgombea wa Chadema, Kalanga alikuwepo akisubiri kunadiwa na mgombea urais huyo ambaye alitumia muda mwingi kumzungumzia Namelock badala ya Kalanga.

Hata hivyo, Lowassa alimnadi Kalanga akimwombea kura kwa wananchi na kumpa nafasi ya kunadi sera zake.

Lowassa aliendelea kufanya hivyo Oktoba 5, 2015 akiwa katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Polisi Monduli mjini ambako aliwaambia wananchi kuwa yeye kama mgombea wa Chadema hawezi kumsaidia mtu wa CCM wakati tayari yuko kwenye basi jingine.

“Najua watachukia sana na hatua hii lakini msiwape kura hata moja,” alisema Lowassa na kumshika mkono Kalanga, kisha akawaambia wananchi, “huyu ndiye mwanangu niliyemteua.”

Kalanga, ambaye alifanikiwa kushinda ubunge wa jimbo hilo, Julai 31 alijiuzulu ubunge na kuhamia CCM huku akisema amechukua uamuzi huo ili kulinda masilahi ya wananchi waliompigia kura.

Alisema ameona akiwa mbunge bila kushirikiana na Serikali hawezi kuwatumikia vyema wananchi.

Waitara na Mbowe

Kama ilivyokuwa kwa Kalanga katika kupiganiwa na Lowassa kushinda ubunge wa Monduli, vivyo hivyo ilikuwa kwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara aliyejiuzulu wadhifa huo na kujiunga CCM, Julai 28. Mwaka 2015 katika kura za maoni za wagombea ubunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Waitara alishika nafasi ya pili.

Matokeo ya kura za maoni katika nafasi ya ubunge, uteuzi wa awali yalionyesha kuwa Nixon Tugara alipata kura 59, Waitara (40), Elly Dallas (15), Deogratias Munishi (8), Lucas Otieno (6), Asia Daudi (5), Deogratias Mramba (5), Gasto Makwetta (1) na wengine watano walipata sifuri.

Hata hivyo, badala ya Tugara kugombea ubunge kutokana na kushinda katika kura za maoni, aligombea Waitara aliyekuwa mshindi wa pili na kuwa mbunge wa Ukonga kabla ya kujiuzulu nafasi hiyo wiki iliyopita.

Baada ya Waitara kuhamia CCM, Mbowe alisema hakushinda kura za maoni, lakini chama kilimbeba hivyo ameikuta Chadema inajengwa na ataiacha inajengwa.

Waitara aligombea ubunge katika jimbo hilo baada ya Kamati Kuu ya Chadema chini ya Mbowe kupitisha jina lake na kumwacha Tugara.

Chanzo: mwananchi.co.tz