Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa: Deni la Sh600milioni limemkimbiza Kalanga

14807 Pic+lowasa TanzaniaWeb

Fri, 31 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Monduli, Julius Kalanga alijiuzulu ubunge baada ya kushindwa kulipa Sh600 milioni alizokopa, hivyo alitaka kusaidiwa kuzilipa.

Akizungumza jana Agosti 30 katika mkutano wa kampeni katika eneo la Mto wa Mbu, Lowassa amedai baada ya Kalanga kupata fedha alinunua ng’ombe ambao walikufa na sehemu nyingine alilima bila mafanikio huku nyingine akizifanyia starehe.

“Naijua taasisi aliyokopa, akaomba alipiwe deni ndiyo akajiuzulu ili apewe nafasi nyingine,” alisema Lowassa.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Kalanga alisema hawezi kulumbana na Lowassa kwa kuwa anamheshimu.

“Nimesikia anasema nilikopa fedha nimeshindwa kulipa, lakini hii mambo ya kukopa ni mambo binafsi, sitaki kumjibu Mzee Lowassa nimewaachia viongozi wa mila, Laigwanani, wazungumze naye kama kweli ananitendea haki,” alisema.

Lowassa alisema sababu alizotoa Kalanga kujiuzulu ikiwamo ile anayosema kuwa Monduli haina maendeleo na haina demokrasia, si za kweli.

“Yeye aseme ameshindwa kuvaa viatu vyangu, aniambie ni wilaya gani imeweza kuleta maendeleo kama Monduli,” alisema.

Lowassa amesema kitendo cha Kalanga kujiuzulu kilikuwa cha ovyo, kimemuudhi na kumkasirisha.

“Kinachoniudhi si kuondoka kwake bali sababu alizotoa kuwa eti Monduli hakuna Maendeleo,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz