Makamu Mwenyelkiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, amewataka watumishi wa umma kufanya mgomo ili kuishinikiza Serikali iwaongezee mishahara.
Lissu ametoa wito huo tarehe 1 Juni 2024, akihutubia wananchi wa Iramba Magharibi, mkoani Singida.
Mwanasiasa huyo amesema kuwa kitendo cha watumishi wa umma kusubiri maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kuiomba Serikali iwaongezee mishahara na marupurupu, hakitawasaidia.
“Nawajua wafanyakazi wa nchi hii walivyo, wote ni ombsomba hawajui kugoma. Wafanyakazi huwa wanagoma wanadai mishahara lakini wa kwetu kila Mei Mosi ombaomba saidia masikini,” amesema Lissu.
Katika hatua nyingine, Lissu amesema kikokotoo kipya cha mafao ya wastaafu kinawapunza wahusika hadi kupelekea baadhi yao kufariki dunia kwa presha ya kusotea fedha zao baada ya kumaliza utumishi wa umma.
Kuhusu wakulima na wafugaji, Lissu amedai utititi wa tozo na ushuru unawafanya waendelee kuwa masikini, na kuishauri Serikali kuwawezesha ili wajikwamue kiuchumi badala ya kusubiri wahangaike kulima na kufuga Kisha ije ichukue kodi.