Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa CCM, Amos Makalla kuitaka Chadema kujisafisha kutokana na kauli ya Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu aliyedai kuwepo kwa fedha zilizomwagwa ili kuharibu uchaguzi wa ndani wa chama hicho, akisema hakuna mtu aliyemwambia amedanganya.
Pia, amesema wanachomwambia angezungumzia kwenye vikao vya ndani vya chama na si kwamba amedanganya.
Lissu alitoa madai hayo Mei 2, 2024 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara mjini Iringa, akiwaonya wanachama wa chama hicho kujiepusha na fedha hizo za rushwa.
Akizungumza na Mwananchi juzi jijini hapa, Makalla alisema kauli hiyo imeonyesha kuwa Chadema ina fedha chafu.
Hata hivyo, akizungumza leo Mei 8, 2024 katika mkutano wa hadhara wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Lissu amesema hakukosea kusema kuwa chama hicho kinanyemelewa na rushwa.
“Nilipokuwa Iringa nimezungumza kwamba, tuwe macho na pesa hizi… kwa sababu zinatumika kuchafua chaguzi zetu, hakuna mtu aliyeniambia nimedanganya, ila wananiambia ungeyasemea ndani.
“Hii rushwa inayoangamiza Taifa inatakiwa izungumziwe ndani, isizungumziwe hadharani?
“Rushwa ni adui wa haki tumeambiwa hivyo. Huyo adui wa haki inabidi akemewe na kupigwa vita kila mahali hasa hadharani ili wananchi wafahamu, lakini kumekuwa na kelele kubwa ajabu,” amesema.
Mbali na CCM, amesema kuna wanachama wa Chadema wanaomshambulia wakimtaka asizungumzie rushwa hadharani.
“Wapo wanaojiita wanachama wenzangu wanasema hayo ukayazungumzie ndani, si hadharani, unachafua chama. Ukizungumza hadharani unasafisha chama, unaonyesha wanachama na Watanzania hatutaki rushwa, ndani ya chama na hatutaki rushwa nje ya chama,” amesema.
Muungano
Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Lissu amesema amekosoa muundo wa Serikali mbili kwa kuwa hautoi fursa sawa akipendekeza muundo wa serikali tatu.
Lissu amezitaja tume ikiwamo ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa na hayati Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1991 kuuliza Watanzania kuhusu vyama vingi, akisema ilipendekeza Muungano wa Serikali tatu.
Nyingine ni tume ya Jaji Robert Kisanga iliyoundwa na Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin Mkapa, nayo ilipendekeza Serikali tatu, lakini mapendekezo hayo yalikataliwa.
“Mwaka 2003 Mkapa akaunda tume nyingine chini ya Jaji Mark Bomani aliyekuwa mwanasheria mkuu wa kwanza Mwafrika wa nchi hii, na yeye akapendekeza Serikali ya Tanganyika, wakakataa,” amesema.
“Jaji (Waziri Mkuu mstaafu) Joseph Warioba naye akasema haiwezekani kuwe na Muungano wa aina hii, lazima kuwe na Serikali ya Tanganyika. Wamekataa,” amesema.
Kabla ya Lissu kuzungumza, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi aliwataka wananchi wilayani humo kujiandaa na uchaguzi kwa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.