Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu aunguruma Chato, azungumzia machungu ya mikataba kuvunjwa

Tundu Lissu Chato Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Wed, 2 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, Tanzania imefunguliwa kesi 10 za kimkataba ambapo kati ya hizo, nne zimeshaamuliwa na Tanzania imetakiwa kulipa mamilioni ya fedha kutokana na kuvunjwa kwa mikataba.

Lissu amebainisha hayo leo Agosti 2, 2023 Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati wa mkutano wake wa hadhara katika wilaya hiyo unaotambuliwa kama kampeni ya “+255 Katiba Mpya, Okoa Bandari Zetu.”

“Kati ya mwaka 2017 na wiki mbili zilizopita, tumefunguliwa kesi 10 na hawa wanaomiliki dhahabu ya nchi hii. Na katika hizo 10, nne zimeshaamuliwa na tumeshindwa zote kwa sababu walikuwa wanaangalia, tunadaiwa Sh847 milioni, sita zilizobaki tunadaiwa zaidi ya Sh2.3 trilioni.

“Na kesi hizo nyingine pia, tutanyolewa bila ganzi kwa sababu mawakili wanapokutana na mawakili wa nje, wanashindwa kujenga hoja, hivyo Tanzania inapoteza kila kesi inayosikilizwa huko nje dhidi ya Tanzania,” amesema Lissu.

Ameongeza kuwa: “Huyu mtoto wenu (Magufuli) ametuingia katika hasara ambayo inaweza kuepukika kabisa, nikiyasema haya nawasema vibaya?” alihoji Lissu huku wananchi wakijibu “hapana” kwenye mkutano huo.

Lissu alisema Tanzania ilikuwa na mashirika zaidi ya 400 wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, hadi anaondoka madarakani mashirika yalikuwa bado yapo. Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, amesema lugha ilianza kubadilika kuhusu mashirika hayo na Rais Benjamin Mkapa alipoingia alianza kubinafsisha mashirika hayo.

Amesema suala la madini wakati wa Mkapa lilikuwa ni gumu, na kwamba yeye mwenyewe alisema kwamba Tanzania haiwezi kuchimba madini hayo badala yake waite wawekezaji ili wachimbe madini hayo.

Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema nchi hii imekuwa na Bunge la ovyo kwa miaka mingi. Amesema nchi imekuwa masikini kwa sababu ya akili za ovyo za viongozi licha ya kuwepo kwa rasilimali nyingi hapa nchini.

Amesema hapa Tanzania kuna madini ya aina mbalimbali kama vile Tanzanite, nickel na mgodi wa tatu kwa ukubwa Afrika ni Geita Gold Mine (GGM) unapatikana mkoani Geita, lakini licha ya utajiri huo, bado nchi hii ni masikini.

“Leo badala ya viongozi wetu kufundisha watu kuchimba nickel, badala ya kufundisha vijana wetu kuchimba dhahabu yetu…wakati wazazi wenu wanawapeleka shule wazazi wenu kuwafundisha panzi ana miguu mingapi, wazungu wanafundisha watoto wao utaalamu wa kuja kumiliki dhahabu yenu, nyie mnabaki manamba,” amesema Heche.

Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema Bunge ni mkutano wa hadhara wa wananchi na mbunge anapokwenda Dodoma atakiwa kuwasemea wananchi wake.

“Mtu mwenye akili timamu ana uwezo wa kuhoji, kubisha, kudadisi, kuuliza na kukataa, huyo ndiyo mtu mwenye akili timamu. Ninazungumza hivyo kwa sababu nina uzoefu wa kukaa bungeni,” amesema Msigwa.

Chanzo: Mwananchi