Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu atoka hospitali, afanya kampeni kwa njia ya WhatsApp

10730 Pic+lissu TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameruhusiwa kutoka hospitalini alipokuwa amelazwa kwa matibabu na baadaye kuhutubia mkutano wa kampeni za udiwani njia ya sauti akiwa nchini Ubelgiji.

Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake Dodoma Septemba 7 mwaka jana.

Baada ya kujeruhiwa, mwanasiasa huyo alitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kisha kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu na baadaye Januari 6 kuhamishiwa Ubelgiji.

Akihutubia mkutano huo wa kampeni, katika kata ya Mawenzi, Lissu aliwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchagua viongozi wanaotoka Chadema ili kuendeleza maendeleo ya mji wa Moshi.

Alitoa hotuba hiyo baada ya kupigiwa simu kwa njia ya mtandao wa WhatsApp na mgombea udiwani wa Chadema katika kata hiyo, Afrikana Mlay wakati wa mkutano huo wa kampeni na sauti ya Lissu ilisikika kupitia spika zilizokuwa kwenye mkutano huo.

Lissu aliwataka wananchi hao kuacha woga na badala yake wajitokeze kwa wingi Agosti, 12 kupiga kura ili kupata viongozi bora.

“Ninawaomba sana wananchi wa Moshi kwa heshima ya mzee (marehemu Phillemon) Ndesamburo, msikubali kurudi Misri,” alisema.

Kutoka hospitali

Awali, Lissu alituma ujumbe wa maandishi akieleza furaha yake ya kuruhusiwa kutoka Hospitali.

Katika ujumbe huo, alioutuma Lissu ameandika:

“Alfajiri ya tarehe 6 Januari ya mwaka huu, niliondoka Nairobi Hospital na kusafiri hadi Leuven, Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu zaidi. Jana tarehe 6 Agosti ilikuwa mwezi wa saba kamili tangu niletwe hapa Ubelgiji kwa ajili hiyo.

Leo tarehe 7 Agosti ni miezi 11 ‘to the day’ (tangu siku) niliposhambuliwa na watu wanaojulikana sana kama ‘watu wasiojulikana.’

Tarehe 7 Septemba mwaka jana sikulala nyumbani kwangu. Tarehe 7 Agosti ya leo, miezi 11 kamili baadaye, nimeamkia nyumbani kwangu.

Tarehe 7 Septemba iliyopita wote mlikuwa na hofu kubwa kama ningemaliza siku hiyo, au siku chache zilizofuata, nikiwa hai. Miezi 11 kamili baadaye, Professor Dk Wilhelmus Jan Mertsemakers, daktari wangu tangu nilipokuja University Hospital Leuven, amesema sina sababu ya kitabibu ya kuendelea kukaa hospitali.

Profesa Mertsemakers amesema nitaendelea na uponyaji nikiwa nyumbani kwangu. Nitatembelewa na homecare nurses (wauguzi wanaotoa huduma nyumbani) kila siku nyumbani kuniangalia naendeleaje. Na nitarudi hospitali kumwona kila baada ya wiki mbili.

Bado nina lichuma kubwa kwenye paja liko kama antenna ya TV za mwaka ‘47. Na Profesa Mertsemakers amesema nitakaa nalo kwa si chini ya miezi sita. Lakini habari ya mujini ndio hiyo: nimetoka hospitalini.

Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuniuguza na kuniponya. Na chochote mtakachokula au kunywa siku ya leo mnibakishie. Siko mbali.”

Chanzo: mwananchi.co.tz