Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu ataka waliotajwa Ripoti ya CAG wawajibishwe

Tundu Lissu Chato Tundu Lissu.

Mon, 29 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, amesema ripoti inayotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka wanaotajwa kuhusika na ufisadi hawachukuliwi hatua kwa sababu wahusika ni baadhi ya viongozi.

Akihutubia mamia ya wananchi mjini Singida baada ya kushiriki maandamano ya chama hicho yanayoendelea katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kushinikiza Katiba mpya, mabadiliko ya kikokotoo na kuchukua hatau kunusuru hali ngumu ya maisha, amesema kila mwaka ripoti ya CAG inaeleza wizi, lakini wahusika hawachukuliwi hatua.

“Kila mwaka tangu nijue kusoma na kuandika sijawahi kuona CAG akitoa ripoti kwamba mwaka huu mahesabu yameenda vizuri, kila mwaka ni orodha ya wizi wa pesa za wananchi, Rais anajua, mawaziri wake wanajua, wakuu wa mikoa wanajua, wote wanajua kwanini hawachukui hatua, unafikiri ni kwanini kama sio wao ndio wahusika," amesema.

Lissu amesema suala la tozo, kikokotoo na kodi ni biashara ya baadhi ya viongozi na ndio maana mambo hayo hata wananchi na watumishi wakipiga kelele hawasikilizwi.

Amesema ili kuondokana na mambo hayo ndio maana CHADEMA imeamua kuanzisha maandamano nchi nzima kudai Katiba mpya ambayo itakuwa ni suluhisho la mambo yote na wananchi kupata haki zao.

“Tunaandamana sababu tumechoka na tusipoandamana CCM hii itatuangamiza si wananchi wa vijijini, mijini pekee yao, lakini ni pamoja na watumishi wa serikali sababu na wao wamechoka, mfano suala la kikokotoo askari, wauguzi, mabwana shamba na watumishi wote kwa ujumla kinawaumiza,” amesema.

Akizungumzia wafanyabiashara wawili wa Mkoa wa Singida ambao ndugu waliotekwa tangu mwaka jana akiwataja kwa majina, amesema ana taarifa kuwa baada ya kutekwa walipelekwa katika Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

“Ndugu wa wafanyabiashara hawa wamekwenda polisi na katika vyombo mbalimbali vya serikali, lakini hawajapata msaada wowote, hivi hawa watu wanaoitwa wasiojulikana wanatoka wapi, kwanini hawa polisi wanapata kigugumizi hawataki hii taarifa kama sio kwamba wametekwa na watu wa serikali,” amehoji.

Kuhusu Soko la Kimataifa la Vitunguu Misuna lililopo katika Manispaa ya Singida, amesema ni aibu kulipa soko hilo jina hilo wakati ukweli halina hadhi hiyo na kuna uchafu.

“Tumepita soko la kimataifa la vitunguu, kimsingi tusiwaambie watu kwamba tuna soko la kimataifa hilo sio soko halistahili hata kuwa soko la mtaa, kata wala manispaa na kama mnaita lile ndio soko la kimataifa basi mkoa huu wa Singida hakuna anayejua masoko yenye hadhi ya kimataifa,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sera Kanda ya Kati, David Djumbe, amesema CHADEMA inafanya maandamano kwa sababu wananchi wamechoka kuibiwa kwenye uchaguzi unaofanyika na kuongozwa na watu wasiozijua shida za wananchi.

"Watu walioshiba huwa hawaandamani, wanaopata huduma nzuri huwa hawaandamani, tunaandamana sababu miaka 60 ya Uhuru na Muungano Serikali ya CCM bado haijatatua kero za wananchi," amesema Djombe.

Wakili wa kujitegemea, Boniface Mwambukusi, amesema wananchi wanataka Katiba mpya itakayoleta uwajibikaji ili kila kiongozi anayefanya mambo ya ovyo achukuliwe hatua.

"Katiba ndio sera na msingi wa mambo yote ya nchi, tunataka Katiba itakayolinda haki za watu na sio hivi sasa ambapo watu wanatekwa na kupotezwa kusikojulikana, tunakata katibu bora ili kuleta mgawanyiko sawia kuwa na Bunge lenye msimamo, sasa hivi tuna bunge ambalo ni bovu na bora livunje," amesema.

Akizungumza katika ibada ya kuliombea taifa, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema serikali imeelekeza mawaziri kuhakikisha hoja za CAG zinajibiwa na hatua madhubuti kuchukuliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live