Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu ataka mabadiliko sheria ya madini

Tundu Lissu Chato Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu

Thu, 7 Sep 2023 Chanzo: Mwananchi

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu, amependekeza maeneo manne ya kubadilishwa kwenye sheria za madini nchini, ili kuwafanya hata wanaomiliki ardhi husika, wanufaike kwa asilimia fulani, na kwamba sheria itamke wazi kuwa madini, pamoja na vilivyomo, ni mali ya wenye ardhi.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa Bunda mkoani Mara, Lissu amesema mbadiliko hayo anayoyapendekeza, lengo ni kuhakikisha wanazungukwa na fursa hiyo, pia wanufaike.

“Sheria ya sasa inasema udongo wa juu anaofanyiwa shughuli za kilimo na mkulima ni mali ya mhusika lakini madini, msimamizi wake ni Rais, sheria inatakiwa iseme wenye ardhi ndiyo wenye madini,” amesema na kuongeza;

“Kukiwa na utaratibu huo, wenye ardhi watafaidika, lakini kwa utaratibu ulipo sasa wenye ardhi ambayo madini yamegunduliwa, hawana chao, lazima wanaondolewa, tena wanaondolewa bila kufuata haki za binadamu.”

Akitolea mfano wa Kijiji cha Mtakuja wilayani Geita, Lissu amesema: “Kijiji kile kilivunjwa mbele yangu, ilikuwa mwezi Machi mwaka 1999, sheria inatakiwa kusema ardhi ni mali ya mwananchi anayeitumia pamoja na vilivyomo na anayegundua madini akubaliane na mwenye ardhi.”

Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema, amesema katika sheria hiyo, kuwekwe kipengele cha namna ya kuchimba, kugawana faida, huku atikaka sheria kuainisha maeneo ambayo yatakuwa kwaajili ya wananchi peke yao.

“Mfano kuna leseni zinazopaswa kutolewa kwa wachimbaji wa kitanzania tu, sasa mwekezaji wa kichina kwenye baadhi ya machimbo anakujaje? Ni kwa sababu watendaji hawajawai kutii sheria yeyote isiyoendana na maslahi yao,” amesema.

Katika maelezo yake Lisu amegusia mgodi wa Nyamongo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini, ambapo amesema wakati Serikali ina asilimia 16 katika mgodi huo, halimashauri husika na vijiji vyake vilivyozunguka na wale waliokuwa na mashamba, hawana umiliki na waliondolewa.

“Jambo lingine la tatu linalopaswa kufanyika, Serikali inapotoa leseni kwa makampuni makubwa, lazima mgawanyo wa umiliki uzingatiwe pamoja na faida zake na kuwafanya wanaozunguka migodi hiyo wanufaike kwa kiasi fulani,” amesema.

Lisu amependekeza eneo lingine linalohitaji kubadilishwa ni kushughulika na umiliki wa madini ambao unampa Rais mamlaka makubwa na kwamba anakuwa hana tofauti na utawala wa kifalme wa Ulaya wa karne ya 61 hadi 17.

Chanzo: Mwananchi