Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu alipuka tena, Serikali yajibu mapigo

Lissu Amuuliza Mbowe Tundu Lissu

Sat, 28 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuwa Serikali imekuwa ikiruhusu usafirishaji wa wanyama kwenda nje ya nchi tangu mwaka 1985, imeiibua Wizara ya Maliasili na Utalii ikisema hairuhusiwi mtu yeyote kusafirisha wanyama.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Eliamani Sedoyeka alisema siku za nyuma sheria iliwaruhusu watu kuvuna wanyama wao wanaowafugia kwenye bustani na kuamua kuwauza nje ya nchi au hata kuwachinja kwa matumizi ya kitoweo, lakini sasa hairuhusiwi.

Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kuwasili nchini juzi, Lissu alisema kuna biashara kubwa ya kuuza wanyama nje ya nchi inafanywa na Serikali na madhara yake ni kuwa siku zijazo watalii watahamia huko wanakofugwa wanyama hao.

“Emirates Sharja wamefungua shamba la wanyama, eneo hilo linalokusanya wanyama mbalimbali ndilo kubwa duniani, miti iliyopo ni zaidi ya 100,000 na wanyama zaidi ya 50,000 kutoka Afrika,” alisema Lissu.

Alidai kuwa hatua ya Serikali ya sasa kuwaondoa Wamasai ni kutoa nafasi kwa Waarabu wa Emirates kuhamisha wanyama wapeleke kwao, “unafikiri wakipeleka wanyama kwao watalii wataenda wapi?”

Hata hivyo, Profesa Sedoyeka ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema: “Hata wewe hapo unaweza kuanzisha bustani yako ukaomba mbegu za wanyama ukapewa, zamani ilikuwa hao wanyama wakizaliana unaweza kuuza au kusafirisha, lakini sio kuuza wanyama wa Serikali, kwa sasa hata wa bustani hawaruhusiwi kusafirisha.” Alisema ndiyo maana hivi sasa Serikali ina mgogoro na wafugaji ambao kwa muda mrefu wamezuiwa kusafirisha, nayo inaangalia namna ya kushughulikia jambo hilo lakini uuzaji na usafirishaji wa wanyama wa Serikali haujawahi kuruhusiwa.

Serikali ilipiga marufuku usafirishaji wa wanyama hao kwa kuwa kuna watu wasio waaminifu walikuwa wakitumia mwanya huo wa ruksa ya wafugaji kuiba wanyama wa Serikali na kuwasafirisha kinyume cha sheria za nchi.

Juni 4, 2022 Serikali iliruhusu usafirishaji wa wanyamapori hai waliokuwa wamesalia kwenye mazizi na mashamba ya wafugaji baada ya zuio lililotolewa mwaka 2016.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 4, 2022 na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), ruhusa hiyo ni kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 6 hadi Desemba 5, 2022.

Hata hivyo, Waziri wa Maliasili na utalii alirejesha zuio hilo ndani ya saa 24 na kusema litadumu mpaka pale Serikali itakapoamua vinginevyo.

Hoja zake nyingine

Katika hotuba yake, Lissu alihusianisha hali ngumu ya maisha na Katiba mpya, akisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kupitisha suala lolote linalohusu fedha kabla ya kujadiliwa na Bunge.

Alisema masuala yote yanayohusu kodi na tozo yalipitishwa kwa ridhaa ya mkuu wa nchi, aliyepewa mamlaka hayo na Katiba tangu Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Hayati Julius Nyerere.

“Kama kweli mmechoka na maisha magumu jibu ni Katiba mpya. Na haitakuwa Katiba mpya isipomnyang’anya Rais mamlaka makubwa aliyonayo.”

Hoja ya Lissu kuhusu hali ngumu ya maisha, inalingana na kilichofafanuliwa na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Longinus Rutasitara akisema imechagizwa na utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Kwa sehemu kubwa sisi (Tanzania) tunazalisha kwa kutegemea nyenzo kutoka nje ya nchi, majanga yaliyoukumba ulimwengu yamesababisha ugumu wa ufikishwaji wa nyenzo hizo na zilizofika zimepandishwa bei, hii imeenda kuongeza na bei ya bidhaa zinazozalishwa,” alisema.

Profesa Rutasitara alisema hali hiyo imekuja taratibu, haikuzuka mara moja, hivyo hata kumalizika kwake kutakuwa kwa mtindo huo.

Hoja ya Lissu kuhusu hali ngumu ya maisha na Katiba, ilipingwa na nguli wa taaluma ya sheria, Profesa Issa Shivji akisema ni vitu viwili visivyohusiana.

“Kwa maoni yangu, haya ni mambo mawili tofauti, gharama za maisha ni masuala ya kiuchumi na hata sababu zake ni za kiuchumi,” alieleza kwa ufupi Profesa Shivji.

Katika mkutano huo wa Lissu, ulishuhudiwa usalama wa aina yake ukiongozwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murillo, jambo lililokuwa nadra kutokea katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, Mhadhiri wa Rasilimaliwatu na Utawala Bora, Dk Lazzaro Swai alisema kilichoshuhudiwa ni dalili njema ya utekelezwaji wa makubaliano katika maridhiano kati ya Rais na vyama vya upinzani.

“Ni dalili itakayolipeleka Taifa letu kwenye mustakabali mzuri wa kisiasa na hata kuongeza chachu ya ushindani badala ya mmoja kuonekana ndiyo mwenye chake na wengine wanasindikiza,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live