Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu akitua tu anaanza na Mwembeyanga

Lissu Chademaaa Lissu akitua tu anaanza na Mwembeyanga

Tue, 24 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati maalumu inayoratibu mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, iliyopewa jina la ‘Lissu Home Coming’, imewaomba wafuasi wa chama hicho na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kesho kumpokea kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mch. Peter Msigwa, Lissu atawasili kesho saa 7:30 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA).

Mch. Msigwa alisema kuwa baada ya kuwasili, Lissu atakwenda moja kwa moja kwenye viwanja wa Mwembe Yanga, Temeke kufanya mkutano wa hadhara kuzungumza na Watanzania.

"Mimi ni mwenyekiti wa kamati ndogo inayotokana na Kamati Kuu ya chama, maarufu Lissu Home Coming, na ndio maana niliondoka Mwanza kuja hapa kwa sababu hiyo ya kushughulikia mapokezi yake kwa kushirikiana na CHADEMA Kanda ya Pwani.

"Na baadhi waliopo katika kamati hii ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani, Baraka Mwago, Grace Kiwelu na mwingine wa Zanzibar.

"Kwa hiyo, niwakaribishe wakazi wa Dar es Salaam tukampokee shujaa wetu uwanja wa ndege na kisha twende Temeke tukamsikilize Lissu maana anafundisha, anaelimisha na tutapata mambo mengi kutoka kwake," Mch. Msigwa alisema.

Lissu aliondoka nchini Septemba 2017 kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi kwenye makazi yake Area D jijini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka bungeni.

Baada ya shambulio, alikimbizwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na baadaye alisafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu kisha kusafirishwa kwenda Ubelgiji ambako aliendelea na matibabu hadi aliporejea nchini kwa mara ya kwanza Julai mwaka 2020, akashiriki Uchaguzi Mkuu akiwania nafasi ya urais kwa tiketi ya CHADEMA.

Novemba 10, 2020, Lissu aliondoka tena nchini, akisindikizwa hadi uwanja wa ndege na Balozi wa Ujerumani kwenda Ubelgiji baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, akidai usalama wa maisha yake ulikuwa shakani.

Januari 13, mwaka huu, Lissu alizungumza na Watanzania kupitia mitandao ya kijamii na kueleza kusudio lake la kurudi nchini Januari 25.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema maandalizi ya kurejea kwa viongozi wote wa chama hicho ambao ni wakimbizi wa kisiasa, yanafanyika kwa hatua mbalimbali.

Alitaja viongozi wengine wanaojiandaa kurejea nchini mbali na Lissu kuwa ni pamoja na Godbless Lema ambaye alikuwa Mbunge wa Arusha Mjini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live