Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu amesema katika uchaguzi ujao hatakubali ‘kuchinjwa’.
Amesema ukimya uliopo juu ya mchakato wa Katiba mpya unamuumiza kichwa, kwani wakienda kichwa kichwa wanaenda kuchinjwa akimaanisha kuenguliwa.
Lissu ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 10, 2023 wakati akiwahutubia wananchi wa Mabibo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mabibo.
Amesema badala ya kuzungumzia Katiba mpya na mfumo mpya wa uchaguzi watu wanazungumzia uchaguzi.
"Mwakani tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, sheria inayotumika ni Ile iliyokuwa ikitumika wakati wa mfumo wa chama kimoja,” amesema Lissu.
Amesema watu wamekuwa wapole sana na upole huo utawapeka machinjioni.
"Mwaka 2019 wagombea wengi walienguliwa kwa kuwa sheria ni ileile na wasimamizi ni walewale, mnafikiri tukienda nini kitakachoenda kufanyika? Huu ukimya wetu juu ya mfumo wa uchaguzi unaenda kutuangamiza, watatupeleka machinjioni," amesema Lissu.
Lissu ambaye alikuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 amebainisha kuwa, watu wameingia hofu na lugha ya Katiba mpya imeanza kupotea.
"Tusiwe tunapuuzia masuala yanayofanywa na Serikali kwa kuwa yanatuhusu moja kwa moja, tunahitaji kuwa na maarifa.
"Kila kitu kinachofanywa na Serikali kinamgusa mwananchi moja kwa moja, Serikali ndiyo inayoweka mzigo wa kodi ambao unamuumiza mwananchi ila siku," amesema.
Mapema, Spika wa Bunge la Wananchi wa Chadema, Suzan Lyimo, amesema waendako mbele ni giza na hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujisajili kwenye mfumo wa kidigitali wa chama hicho.
Pia amewataka kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama na Serikali ili kuleta mabadiliko na kuwatumikia wananchi.
"Tujitokezeni katika operesheni inayoendelea ya kujisajili kwa njia ya mtandao, kwa kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni mwakani tuweze kuchagua viongozi tunaowataka,”amesema Lyimo.