Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu: Utendaji wa Rais Samia utaponya makovu

Lisu Pic2 Data Rais Samia akiwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu amesema mwenendo wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unaonyesha kuwa unakwenda kuyaponya makovu ya mambo mabaya yaliyotokea siku za nyuma.

Lissu alisema katika utendaji kazi wake, Rais Samia amekuwa kiongozi wa kurekebisha mambo mabaya na kutaka mambo yafanyike katika hali ya usawa. Alisema Rais huyo akibaini kuna jambo halikufanyika sawa, analirekebisha.

Kiongozi huyo wa juu wa chama kikuu cha upinzani nchini, aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa akizungumza katika kipindi cha medani za siasa, kinachorushwa na runinga ya Star Tv.

Lissu alifanyiwa mahojiano hayo, kwa njia ya mtandao moja kwa moja akiwa Ubelgiji anakoishi kwa sasa.

Hata hivyo, alipoulizwa ikiwa anaungana na vijana wa sasa wanaosema “mama anaupiga mwingi” ikimaanisha anafanya vizuri sana, Lissu alisema: “Mimi sio mpiga vigerere, lakini kuna mambo Mama (Rais Samia) ameanza kuyafanya vizuri, kwa sababu ameyafanya vizuri, tutaungana naye ili ayafanye vizuri zaidi. Kuna kazi kubwa iliyopo mbele yake ambayo si rahisi, lazima tumpe moyo.

“Lazima tumwambie mama kwenye safari aliyoianza asiogope, unakwenda vizuri na dunia inakuunga mkono na sisi tutakuunga mkono kwenye hii safari ya kusaidiana kuiweka nchi yetu katika misingi bora ya kidemokrasia,” alisema Lissu.

Mwanasheria huyo alitolea mfano namna Serikali ilivyoshughulikia suala Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake kuachiliwa, baada ya kufutiwa mashtaka ugaidi.

Katika maelezo yake, Lissu alisema si yeye peke yake aliyefanikisha Mbowe kuachiliwa kwa kuzungumza na Rais Samia, bali wapo wananchi wengi wakiwamo wa ndani na nje waliopaza sauti zao.

Alisema kesi kubwa ya kisiasa kama ya Mbowe, mara nyingi huwa kunakuwa na jitihada nyingi zinazofanyika ndani na nje ya nchi kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana.

“Mimi ni mmoja kati ya watu wengi tuliomwambia Rais Samia aachane na kesi hii kwa sababu ilikuwa inamchafua, inaichafua nchi, chama chake, Serikali na ilikuwa inaligawa Taifa na inatesa watu,” alisema

Alisema kulikuwa na jitihada kubwa si za viongozi wa kidini pekee, bali hata wanasiasa ambao hawajahi kusemwa.

“Rais aliniambia atalifanyia kazi na amelifanyia kazi. Kwa heshima yake anaifanya sasa Tanzania ielekee katika misingi mipya ambayo mambo mabaya kama haya huenda yasitokee tena, ni vizuri tukasaidiana naye na kumuunga mkono ili asirudi nyuma na kutetereka,” alisema kiongozi huyo.

Apata pasipoti mpya

Akizungumzia suala la hati yake ya kusafiria, Lissu alisema ilipotea alipokuwa Frankfurt –Ujerumani alikokuwa amekwenda kumsindikiza kijana wake aliyekuwa anakwenda Marekani, lakini wakati akirejea Ubelgiji, begi lake lililokuwa na vifaa mbalimbali ikiwemo pasipoti lilikwapuliwa katika Kituo cha treni.

Hivyo, ilimlazimu kuomba hati nyingine kwa njia ya mtandao lakini kwa sababu za hofu kuwa muombaji ni Lissu, alipokutana na na Rais Saamia ilibidi amweleze hana hati ya kusafiria, na angetaja kurejea nyumbani ikiwa ataridhia.

“Rais aliniahidi atalifanyia kazi, nataka niwajulishe kuwa hati yangu mpya ya kusafiria imefikia leo (juzi), hapa Ubelgiji. Rais amelifanyia kazi ombi langu, nachukua fursa hii kumshukuru sana,” alisema Lissu.

Kurejea Tanzania

Kuhusu kurejea Tanzania, alisema kwa sasa anaendelea vema na yupo tayari kurudi muda wowote.

“Tusihesabu tena mwaka, miezi na wiki, nitarudi nyumbani. Nimemuomba Rais afanye kitu kimoja, aseme hadharani kwamba Lissu ‘njoo nyumbani utakuwa salama’…Nikamwambia akifanya hivyo, nitarudi nyumbani.

Alipoulizwa anadhani kwanini hadi sasa Rais hajatamka hilo, Lissu alisema “Rais Samia ana kazi na mambo mengi, sitaki kuamini amekataa kufanya hivyo, kwa sababu aliniahidi kulifanyia kazi.”

Lissu alisema masuala mengine aliyahidiwa na Samia kuwa atayafanyia kazi, yameshatekelezwa, hivyo anaamini hata hilo litatekelezwa muda si mrefu.

Pia alimshukuru kwa kumuahidi kushughulikia mafao na kiinua mgongo chake na fedha za matibabu ambazo hakuzipata wakati akiwa mbunge na aliumizwa kazini.

Atakubali uteuzi?

Alipoulizwa kutokana na mwenendo mzuri wa utendaji wa Rais Samia, ikitokea akamteua atakubali, Lissu alisema hataukubali uteuzi huo.

“Rais akaniteua nimwambia mheshimiwa Rais kumbe hunipendi kiasi hicho? Kama unataka nikusaidie ufanye kazi yako vizuri, naomba uniache niwe huru ili nikwambie mambo yanayokwenda vibaya bila kuogopa kwamba wewe unanilipa mshahara.

“Kwa sababu akishaanza kukulipa mshahara, atakuziba na mdomo hii kitu haitawezekana kabisa…Itakuwa ni kitu kibaya kwa Tanzania kupoteza sauti imara nje ya Serikali,” alisema Lissu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live