Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lipumba awataka wajumbe kuharakisha mikutano ya hadhara

Lipumba Pic Wajumbe Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewataka wajumbe wa baraza kuu la uongozi la chama hicho, kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili kuimarisha chama chao.

Amesema Serikali imeshaondoa zuio la kutofanyika mikutano ya hadhara, sasa ni fursa kwao kutumia nafasi kufanya shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara.

Januari 3, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa vyama 19 vyenye usajili wa kudumu Ikulu, Dar es Salaam, alitangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na mtangulizi wake, hayati John Magufuli mwaka 2016.

Profesa Lipumba ameeleza hayo leo, Jumamosi Januari 21, 2023 akifungua kikao cha siku mbili cha baraza kuu la uongozi kinachofanyika katika ofisi ya makao mkuu ya CUF, Buguruni Jijini Dar es Salaam.

"Wajumbe wa Baraza kuu la Uongozi la Taifa mmepewa fursa sasa katika maeneo yenu kufanya mikutano ya hadhara ili kueleza sera za CUF.

"Pia kueleza msimamo wetu wa haki sawa na furaha kwa wote na sera gani zinazopaswa kutekelezwa ili Tanzania kutumia rasirimali zake kukuza uchumi utakaongeza ajira kwa vijana na kutoa furaha kwa wananchi wote," amesema Profesa Lipumba.

Mbali na hilo, Profesa Lipumba amesema wajumbe hao watajadili na kutoa mapendekezo yao kuhusu upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi, akisema ni muhimu katika mazingira ya sasa ili chaguzi zijazo ziwe huru na haki.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, amesema wajumbe hao watajadili pia suala la mfumuko wa bei na mwenendo wa uchumi na kutoa ushauri na mapendekezo yao kwa Serikali kwa mustakabali wa Taifa.

Awali Naibu Katibu wa chama hicho Bara, Magdalena Sakaya amesema taratibu za kikao hicho kinachofanyika kila baada ya miezi minne zimefuata ikiwemo akidi za wajumbe kutimia.

Chanzo: Mwananchi