Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lipumba akishinda makao makuu kubaki Dodoma

50e3af4ac8373d18ce82b09337b7c3a4 Lipumba akishinda makao makuu kubaki Dodoma

Tue, 15 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema akiingia madarakani makao makuu ya nchi, yataendelea kuwa Dodoma.

Alitoa msimamo huo jana wakati akihutubia wananchi wa Dodoma kwenye mkutano wa kampeni katika Kata ya Tambukareli. Kwa mujibu wa Profesa huyo, hana mpango wa kuhamisha makao makuu ya nchi kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Alisema ameamua hivyo kwa kuwa alishiriki katika mchakato wa wazo la makao makuu ya nchi kuwa katikati ya nchi wakati akiwa mwanafuzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).

"Nikiwa mwanafuzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ndio wazo hili lilibuka ambapo nchi nyingi zilitaka makao makuu yawe katikati ya nchi na mimi nilishiriki, hivyo mkinipa kura Oktoba 28, sitahamisha makao makuu, yataendelea kuwepo Dodoma"alisema Lipumba.

Mwanasiasa huyo pia alisema sera ya CUF inahimiza ‘Haki Sawa Kwa Wote’, hivyo atahakikisha anaboresha sekta ya elimu, na haki ya lishe bora na ya uhakika kwa kila Mtanzania.

Pia alisema atahakikisha haki ya afya bora kwa kila Mtanzania, haki ya kuwa ajira bora yenye ujira bora na kuhakikisha utajiri kwa mapato halali kwa kila mwananchi.

Alitumia fursa hiyo kumnadi Mgombea Udiwani Kata ya Tambukareli, Clinton Mmanzi kuwa ni kijana atakayewasaidia kuwatatulia changamoto za afya na miundombinu.

Mmanzi aliwaomba wakazi wa Tambukareli, wampe kura na kwamba endapo kuna wagombea watawapa fedha, wachukue lakini kura wampe yeye.

Akiwa wilayani Chamwino jana, Profesa Lipumba aliwahakikisha wakulima na wafugaji kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atawatafutia masoko ili wauze kimtandao.

Chanzo: habarileo.co.tz