Nanyamba. Mgombea urais kupitia CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema akichaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi atahakikisha anamaliza changamoto ya ajira nchini Tanzania.
Amesema miongoni mwa ajira atakazotoa ni kuziba nafasi za watumishi wa serikali walioondolewa kwa madai ya kuwa na vyeti feki pamoja na za watumishi waliostaafu na kufariki dunia.
Amedai nafasi hizo hazijajazwa jambo ambalo linasababisha uhaba wa watumishi katika sekta ya afya na elimu.
Ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mji mdogo wa Mahuta Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
"Sasa hivi watu wanasema vyuma vimekaza na hii inatokana na sera ya serikali, wafanyakazi hawajaongezewa mishahara idadi ya wafanyakazi haiongezwi kwenye sekta muhimu kama afya na elimu," amesema Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi.
"Wapo watumishi walioondolewa na serikali kwa madai ya kuwa na vyeti feki lakini nafasi zao hazijajazwa na watu wengine, pia wapo waliomaliza masomo yao ya udaktari hawajapata ajira pamoja na kwamba tuna upungufu wa wauguzi na madaktari. Wapo walimu nao hawajapata ajira pamoja na kwamba hatuna walimu wa kutosha.”