Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lipumba, Maalim Seif uso kwa uso Liwale

20138 Pic+lipumba TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umeelezwa kuchukua sura mpya baada ya pande mbili zinazovutana kutikiswa na mgombea ubunge wa chama hicho huko Liwale, Mohammed Mtesa.

Hali hiyo inatokana na kauli ya kumuunga mkono Mtesa iliyotolewa na upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, huku upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ukishangazwa na uamuzi huo.

Mgogoro ndani ya CUF ulianza baada ya Lipumba kurejea katika uongozi mwaka 2016, ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipojiuzulu .

Jambo hilo liliibua mgogoro wa uongozi baada ya ofisi ya msajili kutangaza kumtambua Lipumba kama mwenyekiti na kusababisha pande hizo mbili kukimbilia mahakamani na kufungua kesi kadhaa ambazo zinaendelea.

Uchaguzi wa Liwale Oktoba 13,

Awali, Mtesa alipitishwa na vikao kuwania ubunge na katika ufunguzi wa kampeni Lipumba alishiriki, lakini juzi upande wa Maalim Seif ulibainisha kuwa unamuunga mkono Mtesa kwa kuwa yupo upande wao.

Upande huo ulibainisha kuwa katibu mkuu huyo atafunga kampeni Oktoba 12.

Akizungumza na Mwananchi, mbunge wa Kilwa (CUF) ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Lindi, Suleiman Bungala ‘Bwege’ alisema ndiye anayeongoza kampeni hizo akishirikiana na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa Salumu Barwani.

Bungala alisema mgogoro baina ya upande wa Profesa Lipumba na Maalim Seif haujakwisha kwa sababu kesi bado iko mahakamani lakini wanaunganishwa na mgombea huyo.

“Mgogoro bado upo lakini tunaunganishwa na mgombea wetu kwenye uchaguzi huu. Huyu mgombea yuko upande wa Maalim Seif, lakini kwa sababu anakubalika sana Liwale, upande wa pili wakamchukua, nasi tukaona hatuna budi kumuunga mkono,” alisema Bungala.

Bungala alisema awali upande wa Profesa Lipumba ulitoa masharti kwamba yeyote anayetaka kwenda kusaidia kampeni za mgombea huyo lazima awe na barua kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Magdalena Sakaya.

Hata hivyo, alisema sharti hilo liliondolewa kutokana na nguvu ya baadhi ya wanasiasa, akiwamo yeye kwa kuwa hawakuwa na kibali hicho.

Juzi katika taarifa yake, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Mbarala Maharagande alisema wanafanya maandalizi kwa ajili ya mapokezi ya Maalim Seif ambaye anatarajiwa kufunga kampeni hizo.

Kwa upande wake, Magdalena Sakaya alisema ana mashaka na uamuzi wa Maalim Seif kufunga kampeni hizo.

Alisema mara kwa mara Maalim Seif na timu yake wamekuwa hawaungi mkono wagombea wanaoteuliwa na upande wa Profesa Lipumba badala yake wanashirikiana na Chadema.

“Maalim Seif hana dhamira ya kweli katika kampeni hizo anakwenda kuharibu. Nia yao siyo nzuri na sisi hatutakubali kitendo cha Maalim Seif kwenda katika kampeni hizo,” alisema Sakaya ambaye ni mbunge wa Kaliua.

“Endapo akienda atakutana na nguvu ya Katiba ya CUF (yaani wananchi) na kitakachowapata wasishangae. Kama wao wanatumia nguvu kubwa kukibomoa sisi tutatumia Katiba.”

Alisisitiza kuwa malengo ya upande wa Maalim Seif si mazuri katika uchaguzi kwa sababu kuna rekodi za maelezo ya nyuma kuhusu kuhusishwa kuondoka CUF na kuhamia Chadema.

Sakaya ambaye aliteuliwa kuwa kaimu katibu mkuu baada ya Maalim Seif kutofika ofisini Buguruni, alisema kazi zote anazifanya yeye baada ya kiongozi huyo kususa, hivyo CUF haitakubali kiongozi asiyefuata Katiba apande jukwaani na kumnadi mgombea wao.

“Siku zote walikuwa wanashirikiana na Chadema katika chaguzi zilizopita leo hii wanasema wanataka kufunga kampeni za Liwale, hatutakubali! Wameona Chadema wamesusia wameamua kurudi huku, lengo lao siyo nzuri na chama kitakaa kikao kujadili suala hili,” alisema Sakaya.

Chanzo: mwananchi.co.tz