Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lijualikali, Kiwanga watoka rumande

Lijualikali, Kiwanga watoka rumande

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Wabunge wawili wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombero) pamoja na wenzao saba wamekamilisha masharti ya dhamana leo Ijumaa Machi 8, 2019.

Hali hiyo imejitokeza baada ya jana Alhamisi washtakiwa hao licha ya kupata dhamana, lakini walijikuta wakirudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo.

Wabunge hao na wenzao wamekaa rumande zaidi ya wiki mbili baada ya upande wa Jamhuri kuweka pingamizi la dhamana tangu walipofikishwa kwa mara kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Februari 25, 2019.

Akizungumza na Mwananchi mara baada ya kukamilisha kwa taratibu zote za dhamana hiyo, leo Alhamisi, wakili wa washtakiwa Hekima Mwasipu amesema wamekamilisha taratibu zote na kufanikiwa kuwadhamini washtakiwa wote.

Mwasipu amesema hakimu anayeendesha kesi hiyo, Elizabeth Nyembele alitoa masharti ya dhamana kwa kila mshtakiwa ametakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayewasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani si chini ya Sh5 milioni na pia atakayeweza kutoa dhamana ya Sh3.7 milioni.

“Wabunge wawili Susan Kiwanga, Peter Lijualikali na wenzao saba wote kwa pamoja leo wamepata dhamana baada ya jana kushindikana kutokana na utaratibu wa dhamana kutokamilika kutokana na masharti yaliyowekwa na hakimu,” amesema Mwasipu.

Baada ya taratibu wa dhamana kukamilika, Kiwanga amesema amewashukuru wanachama, viongozi na timu ya mawakili kwa umoja wao kuhakikisha wanapambana na kupata dhamana leo.

Amesema kesi wanayoshtakiwa mahakamani hapo tayari ilifutwa baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta ushahidi wa kutosha.

“Sisi ni viongozi katika majimbo yetu na kesi hii kimsingi ilifutwa kutokana na Jamhuri kusuasua kuleta mashahidi mahakamani ndio maana hakimu aliifuta ile kesi,” amesema.

 Naye Lijualikali amesema kesi inayowakabili ina lengo la kuwadhoofisha kisiasa pamoja na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye amekaa mahabusu zaidi ya miezi mitatu gerezani.

Lijualikali ametoa pole kwa vijana wa kijiji cha Sofi kutokana na kukipigania chama na kuwataka Watanzania kukataa dhulma na wanakataa dhulma kwa sababu ya kizazi cha watu wenye kutaka mabadiliko.

Wabunge hao na wenzao saba wanashtakiwa mahakamani hapo kwa kesi ya jinai namba 43 ya mwaka 2019, ilidaiwa kwamba Novemba 26, 2017 walitenda makosa manane likiwemo la kuharibu mali na kuchoma moto ofisi ya Serikali ya kijiji cha Sofi wilayani Malinyi.



Chanzo: mwananchi.co.tz