Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Leo ni leo hatima maombi ya kina Mdee

Mdee Mak.jpeg Leo ni leo hatima maombi ya kina Mdee

Wed, 22 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maombi ya wanachama 19 wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kibali cha kupinga kufukuzwa uanachama, yatajulikana leo Mahakama itakapotoa uamuzi wa pingamizi walilowekewa na chama hicho.

Halima Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake 18, wamefungua maombi, Mahakama Kuu Dar es Salaam, wakiomba kibali cha kupinga uamuzi wa chama hicho kuwavua uanachama.

Wajibu maombi ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Chadema kupitia jopo la mawakili wake linaloongozwa na Peter Kibatala wameweka pingamizi wakiiomba Mahakama hiyo isiyasikilize maombi hayo, wakidai kuwa yana kasoro za kisheria huku wakibainisha hoja sita.

Pingamizi hilo lilisikilizwa na Jaji John Mgetta, Juni 13, mwaka huu na baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alipanga kutoa uamuzi wake leo.

Uamuzi huo ndio utakatoa hatima ya usikilizwaji wa maombi ya kina Mdee ya kupewa kibali kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wao.

Kama Mahakama haitakubaliana na hoja za pingamizi la Chadema, basi italitupilia mbali pingamizi hilo na itaendelea na usikilizwaji wa maombi ya msingi ya kina Mdee ya kupewa kibali.

Iwapo Mahakama hiyo itakubaliana na hoja za pingamizi la Chadema, basi itayatupilia mbali maombi hayo ya kina Mdee.

Hata hivyo, aina ya amri ya kuyatupilia mbali maombi hayo itakayotolewa haitakuwa ya kuwafungia milango moja kwa moja, bali watakuwa na fursa ya kuyafungua upya baada ya kurekebisha kasoro ambazo itakuwa imeziainisha.

Wengine waliofukuzwa ni Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Hoja za pingamizi

Maelezo ya waombaji si halali kwa kusainiwa na mawakili pamoja na waombaji; badala ya waombaji tu na sehemu ya uthibitisho kwenye maelezo kwa kusema wanathibitisha taarifa za kwenye kiapo badala ya maelezo ya waombaji.

Viapo vinavyounga mkono maombi hayo si halali, kwa kujumuisha maoni na hoja badala ya taarifa za ufahamu wao na pia kuwepo saini za nawakili badala ya saini za waombaji pekee.

Kukosea jina la taasisi ya Chadema inayopaswa kushtakiwa, kwa kuitaja kuwa Bodi ya Wadhamini wa Chadema (Bord of Trustee of Chadema), badala ya Bodi ya Wadhamini, Chadema, iliyosajiliwa (The Registered Trustee).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live