Halmashauri kuu ya taifa ya Chama cha Mapinduzi (Nec) inatarajia kukutana leo Novemba 13, 2022 jijini Dodoma ili kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama walioomba uongozi wa chama katika ngazi ya mikoa na taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Novemba 12, 2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka, kikao hicho kimetanguliwa na kikao cha kamati kuu kilichokutana leo na kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Pamoja na mambo mengine vikao hivi vitakuwa na kazi ya kupokea mapendekezo, kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama walioomba uongozi katika ngazi ya mikoa na taifa kwa upande wa jumuiya pamoja na Chama,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha halmashauri kuu ya CCM taifa kitapitisha majina ya wanachama wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wa chama hicho.
“Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, leo Dodoma. Kikao hiki ni maandalizi ya kikao cha Nec kitakacho fanyika kesho,” amesema Shaka katika taarifa yake.
Vikao hivyo ni mwendelezo wa mchakato wa kutafuta viongozi wapya wa CCM kupitia uchaguzi wa Chama ambao tayari umeshakamilika katika ngazi ya shina, tawi, kata na wilaya.