Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lembeli azidi kuwapasua vichwa viongozi wa CCM

9816 Lembeni+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahama. Zikiwa zimepita takribani siku 10 tangu mbunge wa zamani wa Kahama, James Lembeli kutangaza kuhama Chadema na kurejea CCM, baadhi ya viongozi wa chama tawala wamesema hawajamkataa mwanasiasa huyo bali anatakiwa kufuata taratibu.

Wiki hii kwenye vyombo vya habari zilikuwapo habari mbalimbali kwamba Lembeli baada ya kutangaza kurejea CCM amekataliwa kwa madai amerudi bila kufuata taratibu za vikao vya chama ambako anapaswa kupitia kupeleka barua ili ijadiliwe.

Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kadati, Kata ya Bulungwa Halmashauri ya Ushetu, Tito Kumbakumba alisema Lembeli alipeleka barua ya kurejea kwenye chama Jumatatu ya wiki hii.

Alisema kwamba wakati anapeleka barua pia kulikuwa na kikao cha halmashauri ya tawi kilichokuwa kimehusisha wajumbe wa kamati ya siasa ya tawi ambao walionyesha nia ya kumpokea.

“Lembeli hata kabla hajahamia Chadema, tawi lake lilikuwa la Kadati, hivyo hata alipoleta barua ya kurejea wajumbe walifurahi sana kwa mwanachama mwenzao kurejea na Ijumaa (jana) ndipo tutaandika muhtasari rasmi wa kupeleka CCM ngazi ya kata kwa hatua zingine,” alisema Kumbakumba.

Akizungumza kwa njia ya simu, Lembeli alisema: “Mimi ni mkongwe kwenye siasa hivyo nazijua taratibu zote za kuhama na kurejea kwenye chama hivyo nilizizingatia.”

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Kahama Joachim Simbira ambaye awali alitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hatambui kurejea kwa Lembeli, sasa amesema hakuwa na maana ya kumkataa isipokuwa hakuwa na barua inayomtambulisha kurejea.

Chanzo: mwananchi.co.tz