Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lema asema waletwe wote

Glema Godbless Lema

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MWENYEKITI wa Kanda ya Kaskazini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amejitapa kushinda ubunge hata akishindanishwa na watia nia wote waliochukua fomu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Lema amesema kama sheria ingeruhusu, angetaka wagombea wote wa CCM Arusha Mjini ashindane nao na kutamba kuwa angewashinda kwa kishindo.

Lema ambaye anatetea nafasi yake kwa awamu ya tatu mfululizo, aliyaeleza hayo jana kupitia ukurasa wake wa Twitter.

“Nimesikia sikia majina ya wagombea ubunge Arusha Mjini kupitia CCM. Kama sheria ingeruhusu, wote 30 wangekuja kushindana nami na picha zao wote kutokea kwenye karatasi ya kura dhidi yangu, bado wangeimba wimbo walioimba 2010 na 2015. Twendeni mpaka mwanzo wa bahari, wepesi sana hawa,” aliandika Lema kwenye ukurasa wake wa twitter.

Vilevile kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, Lema aliwaambia wakazi wa Arusha hususani Jimbo la Arusha Mjini kwamba, watashinda.

“Tuna washinda tena. Msiogope,” Lema aliwatia moyo wapigakura na wapenzi wa CHADEMA na wananchi wa jimbo lake.

CCM jana walifungua pazia kwa wanachama wake kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo na miongoni mwa waliochukua fomu ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM unatarajiwa kukamilika Julai 17, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live