Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lema ahamasisha uchangiaji fedha viongozi Chadema wakikutwa na hatia

98599 Hukumu Kinambowe+pic Lema ahamasisha uchangiaji fedha viongozi Chadema wakikutwa na hatia

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwatia hatiani  viongozi nane wa Chadema na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho Dk Vincent Mashinji, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema wanaanza kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa faini.

Faini hiyo ambayo ni zaidi ya Sh100 milioni inalipwa baada ya washtakiwa wote tisa kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 ikiwemo uchochezi.

Uamuzi wa kuwatia hatiani umetolewa leo Jumanne Machi 10, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama  hiyo, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande  wa mashtaka na ule wa utetezi.

Akizungumza baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Lema amesema ni lazima kutafuta fedha hizo ili kuzilipa, kwamba wananunua uhuru wao ili kuepuka kwenda jela.

“Uhuru wao ni bora kuliko kwenda jela tutakwenda kuzitafuta fedha hizo. Faini ni kubwa lakini hatuna jinsi," amesema Lema.

Naye diwani wa Tabata, Patrick Assenga amesema faini ni kubwa lakini Chadema ni taasisi watahakikisha wanachangishana miongoni mwa wanachama ili kuhakikisha fedha hizo zinapatikana haraka.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Nina uhakika viongozi wetu wa juu watakaa na kutulia kwa ajili ya kukata rufaa kulingana na hukumu hii. Tunashukuru tumepokea uamuzi wa hakimu lakini tutakwenda kukata rufaa," amesema Assenga.

 Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema ingawa hakimu amejitahidi lakini faini iliyotolewa ni kubwa hasa ya fedha katika mazingira ya sasa akisema kuna kesi nyingine zinahitaji majawabu ya kisiasa.

"Historia imeandika lakini wanasheria watatuongoza zaidi lipi la kufanya katika hatua hii," amesema  Mbatia. Hata hivyo, muda mfupi baada ya mahakama kuwatia hatiani washtakiwa hao, ndugu, jamaa na marafiki waliopo ndani ya mahakama hiyo walianza kulia kimya kimya huku wakifuta machozi. Mbali na Mbowe na Dk Mashinji, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika; Naibu Katibu Mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa. Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Chanzo: mwananchi.co.tz