Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lema: Sitagombea tena Kanda ya Kaskazini uchaguzi ujao

Lema Pic Bandari Godbless Lema

Thu, 30 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini anayemaliza muda wake, Godbless Lema amesema hatagombea tena uchaguzi ujao wa kanda hiyo unaotarajiwa kufanyika Julai mwaka huu.

Lema ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na amekuwa mwenyekiti tangu mwaka 2019, ametoa msimamo huo leo Alhamisi Mei 30,2024 kupitia akaunti yake ya mtandao wa X zamani Twitter.

Katika mtandao huo, Lema ameandika, “kwa ajili ya ustawi wa chama changu na uimara wake katika kujenga misingi bora na muhimu haswa katika kipindi hiki tunachoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji na Uchaguzi Mkuu 2025, sitagombea nafasi ya mwenyekiti wa kanda kwa mara hii katika uchaguzi unaokuja.

“Kwa sasa nitafanya wajibu wangu muhimu wa ujenzi wa chama katika kipindi kilichobaki,”ameandika Lema ambaye ni mbunge za zamani wa Arusha Mjini kwa miaka 10.

Msimamo huo wa Lema umekuja siku moja baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kushindwa kutetea kiti chake mbele ya Joseph Mbilinyi maarufu Sugu katika uchaguzi uliofanyika jana Mei 29 2024 Makambako mkoani Njombe.

Katika uchaguzi huo, Sugu alimshinda Mchungaji Msigwa kwa kura 54 dhidi ya 52 alizozipata mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa Lema alitumia ukurasa wake wa X kuandika, “nimefurahi nilipoisikiliza hotuba yako (Msigwa) baada ya uchaguzi wa kanda ya Nyasa kumalizika, umesema thamani yako sio cheo, what you actualy mean, leadership is not a title fantastic message.

“Na pia muhimu zaidi umesisitiza kuendelea kuwa mwanachama senior wa chama na upo tayari kutumwa popote ku share nguvu na uzoefu wako, jambo la baraka sana.

“Hautakuwa mpweke kwa muda mrefu sana katika club ya wanachama senior, watu wengi tutaungana na wewe katika siku za hivi karibuni, pengine kwa style tofauti,”ameandika Lema.

Mwezi uliopita Mwananchi Digital ilizungumza na Lema ikitaka kujua msimamo wake endapo atagombea tena nafasi, akatoa ahadi kwamba ataweka wazi suala hilo Mei mwaka huu, jambo alilolitimiza.

Mwananchi ilimtafuta Lema kutaka kujua kitu gani anajivunia kwenye uongozi wake aliodumu nao kwa miaka mitano.

Kupitia ujumbe mfupi mwanasiasa huyo akajibu,“kuwa imara katika ujenzi wa demokrasia hata tulipopita katika majaribu ya mateso na… jambo ambalo limezaa vijana wengi wanaofahamu sasa makusudi ya safari yetu katika ujenzi wa Taifa la haki.”

Chanzo: Mwananchi