Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumekucha uchaguzi mdogo Mbeya Mjini

12725 UCHAGUZI+PIC TanzaniaWeb

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kumekucha uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata nne za Jiji la Mbeya. Vyama vya CCM na Chadema vimewatangaza wagombea wao huku CCM wao wakiwarudisha waliofukuzwa na Chadema ili kutetea tena kinyang’anyiro hicho.

CCM wao imewarudisha waliokuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kufukuzwa kwa kile kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu ambao ni Geofrey Kajigili (Sisimba), Newton Mwatujobe (Maanga), Mchungaji David Ngogo (Nsalaga) na Hamphrey Ngalawa (Iwambia).

Akizungumza na gazeti hili leo katika ofisi za chama hicho, katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Gerrald  Mwadallu amesema   wagombea hao  tayari wamekabidhiwa barua za utambulisho zitakazopelekwa  kwa watendaji wa kata na wanatarajia kuanza kampeni  za kuwanadi Agosti 24, 2018.

"Tuna uhakika hawa wagombea wetu ni wachapa kazi na wanatambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM chini ya Rais wetu John Magufuli.

“lakini kule walikokuwa walifanyiwa mizengwe kisa tu wanaunga jitihada za viongozi wa CCM. Lakini sisi tunawarudisha hawa tukiamini bado wanahitajika na wananchi wa kata husika, tunaomba waturudishie watu hawa kwa maendeleo zaidi,” amesema Mwadalu.

Kwa upande wa Chadema Mbeya Mjini, tayari kimewapitisha wagombea wake kupitia kamati tendaji ya chama hicho baada ya kupigiwa kura za maoni na wajumbe wa kata husika.

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu amewataja wagombea wao na kata katika mabano ni Steven Mwashilindi (Maanga), Elisha Mwandele (Iwambi),  Odinary Sanga maarufu Pablo (Sisimba) na  Reward Mshanga.

Mwaipalu amesema tayari wagombea hao juzi  walitambulishwa rasmi kwa wananchi wa kata husika na sasa wanachosubiri ni kuanza kwa kampeni.

 “Kamati tendaji wilaya imezingatia matamanio ya wajumbe waliopiga kura kwenye kata lakini imeonyesha wagombea walioshinda kwenye kura za maoni wanapigiwa chapuo kubwa na wananchi wenyewe.

“Hivyo na sisi tulipopitia sifa na uwezo wa kila mmoja kulingana na kura walizopata, tuliridhika kwamba walioshinda kwenye kura za maoni ndiyo wanaofaa zaidi kuwakilisha chama chetu kwenye kinyang’anyiro hicho,” amesema. 

Uchaguzi huo wa Septemba 16, 2018 utahusisha  majimbo matatu ya Ukonga, Monduli na Korogwe Vijijini na na kata 21 nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz