Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea atua ACT Wazalendo, Lema ashinda kura za maoni

C4d78e267541bcce59bef0c709b10dc0.png Kubenea atua ACT Wazalendo, Lema ashinda kura za maoni

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ALIYEKUWA Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea amejiunga na Chama cha ACT – Wazalendo, huku aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameshinda kura za maoni .

Kuhusu Kubenea, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa ACTWazalendo, Janeth Rithe alithibitisha kupokelewa kwa Kubenea katika chama hicho.

Kubenea na wanachama wengine walijiunga jana na kupokewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad. Akihojiwa, Kubenea alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa mgumu, kwa kuwa katika maisha yake hicho ni chama cha pili kujiunga.

“Nilifika mahali nikasema kwamba kama Maalim Seif alianzisha CUF kwa jasho na damu akaondoka baada ya kutoridhika na hali iliyokuwa inaendelea kwenye chama hicho, akaondoka… sembuse mimi. Ni lazima safari ya mabadiliko iendelee,” alisema Kubenea.

Rithe alisema kuwa kujiunga kwa Kubenea ni mwendelezo wa harakati zao kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu. “Kama mlivyoshuhudia jana (juzi) tulimkabidhi fomu ya urais aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe baada ya kujiunga na chama chetu. Huu ni mwanzo. Wapo wengi wanakuja,” alisema Rithe.

Alisema chama hicho kupitia kwa Maalim Sharif kinaendelea na vikao katika baadhi ya majimbo hususani mkoani Dar es Salaam, kuona jinsi watakavyoweza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu.

Wakati huo huo, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema ameshinda katika kura za maoni za ubunge kugombea jimbo hilo jana, baada ya kupata kura 181 dhidi Ally Bananga aliyepata kura 22. Msimamizi wa Uchaguzi, Michael Kilawila alisema kuwa kinyang’anyiro hicho kilikuwa na wagombea wanne, ambapo wawili walipeleka barua za kujiondoa hivyo wakabaki Lema na Bananga.

Akijinadi kwa wapiga kura jana, Lema alisema “huwezi kuwa na mgombea ubunge ambaye hawezi kujua madiwani ni akina nani.” Kwa upande wake, Bananga alisema wazazi wake ni wanaCCM lakini undugu wake na wanachama hao hauathiri jambo lolote katika chama.

Chanzo: habarileo.co.tz