Dodoma. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema bado kuna shida ya umeme jijini Dar es Salaam kutokana na kukatika mara kwa mara huku akiitaka Serikali kutoa majibu ya jambo hilo.
Kubenea ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 24, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza huku akiyataja maeneo ya Kigamboni, Ukonga, Ubungo na Kibamba kuwa na tatizo hilo la kukatika kwa umeme licha ya mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi kuwa katika maeneo hayo.
Akijibu swali hilo la nyongeza, naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema hali ya kukatika kwa umeme si kubwa kama ilivyokuwa mwanzo.
Kuhusu kutoa taarifa ya kukatika kwa umeme, Mgalu amesema huwa zinatolewa kupitia makundi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp yaliyoundwa katika kila kandana kwamba hata yeye yupo katika kundi la wadau wa umeme eneo la Kibamba.
Katika swali la msingi, mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amehoji ni kwa nini jimbo la Kibamba umeme unakatika mara kwa mara huku akishangazwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutopunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wateja wake waliopo maeneo ya mbali.
Akijibu swali hiyo Mgalu amesema kukatika umeme Kibamba kunatokana na kuhamisha miundombinu ya umeme ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro -Dar es Salaam.
Pia Soma
- Ushauri wa Mbatia kwa Dk Kigwangalla kuhusu Bodi ya Utalii
- Mashauri 8,489 yapokelewa Zanzibar
- Kituo cha afya, gari la wagonjwa vyaimarisha huduma Madaba