Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea achambua tuhuma za Meya Dar

91627 Pic+kubenea Kubenea achambua tuhuma za Meya Dar

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mjumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, Saed Kubenea amedai tuhuma tatu kati ya nne alizokuwa akituhumiwa meya wa jiji hilo, Isaya Mwita hazina mashiko.

Januari 9, kamati iliyoundwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, iliwasilisha taarifa ya uchunguzi dhidi ya Mwita anayetuhumiwa kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari la ofisi ambalo alipata nalo ajali na kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubungo Boniface Jacob kugombana na wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

Kubenea alitoa uchambuzi huo jana huku akisisitiza bado wanamtambua Mwita kuwa ni meya wa jiji hilo, akisema wasiomtaka wana njia mbili za kumuondoa lakini si ule mchakato uliofanyika Januari 9. “Wanaweza kuanza upya mchakato ili kumuondoa Mwita na njia ya pili ni kumshawishi Rais John Magufuli avunje jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Fedha za Uda

Kubenea ambaye pia ni mbunge wa Ubungo (Chadema) akizungumzia tuhuma za Sh5.8 bilioni alisema fedha hizo zilishatumika kabla kamati ya kumchunguza Mwita haijaundwa.

Alisema kwa nyakati tofauti baraza lilipitisha azimio la kutotumia fedha za Uda kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutoridhika na mwenendo wa uuzwaji wa Uda na miradi iliyokuwa ikiletwa na ofisi ya mkurugenzi haikuwa ikikidhi matakwa ya kutumika kwa fedha hizo.

“Tulikataa fedha hizi zisitumike kwenye miradi mbalimbali ya kupanua stendi ya mkoa Ubungo kwa Sh3 bilioni, ununuzi wa mabasi ya utalii kwa jiji la Dar es Salaam. Yaani Chadema itoe fedha kwa ajili ya mabasi ya utalii.”

“Badala ya kumpongeza Mwita na baraza kwa kuzuia fedha zisitumike kwenye miradi hiyo, leo wanataka kumuondoa. Hizo fedha hazikuwa Sh5.8 bilioni bali Sh3.6 bilioni lakini baada ya kuweka katika akaunti maalumu zikaongezeka,” alisema Kubenea.

Alisema kuna haja ya uchunguzi maalumu kufanyika katika ofisi ya mkurugenzi ili kubaini alichodai kuwa ni madudu mengi katika ofisi hiyo.

Kuhusu tuhuma za Mwita kushindwa kuongoza kikao cha baraza hilo na kusababisha ugomvi kati ya Jacob na Chaurembo, Kubenea alisema si kweli kwa sababu aliyeanzisha ugomvi huo ni meya wa Temeke aliyetaka kupora sanduku la kura baada ya mjumbe wa CCM kumpigia kura mgombea wa upinzani.

“Aliyeshtaki ndiye mtuhumiwa, Chaurembo asituchoshe aishie hapo, hana mamlaka kuzungumzia maadili ya utumishi wa umma,” alisema.

Mwananchi lilimtafuta Chaurembo kutaka maoni yake kuhusu hoja hizo na alijibu kwa kifupi “aliyetakiwa kunidhibiti ni Mwita.” na kukata simu.

Ni abiria au dereva?

Akizungumzia matumizi mabaya ya gari la ofisi hiyo, Kubenea alisema Mwita haendeshi chombo hicho bali ni dereva aliyeajiriwa na ofisi ya mkurugenzi wa jiji, huku akifafanua moja ya kosa lililotajwa ni gari hilo kumgonga mwendesha pikipiki.

“Hivi kesi ya trafiki unamshtaki abiria? Anayeshtakiwa dereva. Lakini kwenye kamati inayoshughulikia nidhamu jambo hili halijaletwa?

“Mkurugenzi wa Jiji, ndiye anayemsimamia dereva na ameshindwa kuleta mashtaka kwenye kikao,” alisema.

Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sipora Liana alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani kujibu tuhuma za Kubenea, alipokea simu na mwandishi alipojitambulisha jina na kueleza anatoka Mwananchi akakata simu.

Mkutano maalumu wa baraza ulifanyika hivi karibuni ukiwa na ajenda ya kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma dhidi ya Mwita kisha kutoa uamuzi wa kupiga kura za kutokuwa na imani na meya huyo huyo aliyehudumu nafasi hiyo tangu Machi 2016.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 18 kati yao 16 wa CCM walipiga kura kutokuwa na imani na utendaji kazi wa Mwita wakati wajumbe wawili wa Chadema hawakupiga kura.

Baadaye wajumbe wa CCM walitangaza azimio la kutokuwa na imani na Mwita likiwa limepitishwa kwa kura 16, lakini wajumbe wa Chadema walisisitiza Mwita bado meya kwa kuwa akidi haikutimia ya kumuondoa.

Kanuni ya 84(1) za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zinaeleza ili kumwondoa meya kwa sababu zozote zile, lazima kuwapo na theluthi mbili ya wajumbe wote. Baraza hilo lina wajumbe 26 na theluthi mbili yake ni 17 lakini siku ya uamuzi kura zilizomkataa Mwita zilikuwa 16. Tayari ofisi ya mkurugenzi wa jiji hilo, imemnya’ang’anya gari Mwita na kumpa siku 14 kukabidhi ofisi hiyo lakini mwenyewe alisisitiza kuwa bado kiongozi akimtaka Liana leo kumpelekea usafiri huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz