Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kofia mbili kuchomoza mabadiliko CCM

Kofipic Data Kofia mbili kuchomoza mabadiliko CCM

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

CCM imeitisha mkutano mkuu maalumu kufanya marekebisho ya katiba yake kwa kuwapa majukumu wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kuwarejesha kwenye NEC makatibu wa mikoa na kofia mbili kwa nafasi za uongozi wa juu.

Haya ni mabadiliko ya 17 kufanyika ndani ya chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (Tanu) cha iliyokuwa Tanganyika, na Afro-Shiraz cha Zanzibar.

Mabadiliko ya mwisho yalifanyika mwaka 2017 yaliyoendana na kuwapunguza wajumbe wengi kwenye vikao vya juu vya chama sababu kubwa ikitajwa ni gharama ingawa kulikuwa na nyingine zilizotajwa nyuma ya pazia.

Hata hivyo, mkutano huu unaotarajiwa kufanyika Aprili mosi pia kuna wana-CCM watatu wenye kesi ya ukosefu wa maadili mbele ya chama na Kamati Kuu imeagiza waitwe kujieleza, akiwamo Humphrey Polepole aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa na Rais na sasa ameteuliwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Mkutano mkuu maalumu wa mwaka 2017 uliowafukuza uanachama wana-CCM 12 na wengine kuonywa, pia ulimpa onyo Dk Emmanuel Nchimbi ambaye baadaye aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Brazil, wengine ni wabunge Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga). Huenda mkutano huu unakuzungumzia hatma ya wana-CCM hao.

Taarifa ya mwisho ya CCM iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ilisema Kamati Kuu iliagiza wabunge hao waitwe kujieleza kutokana na dosari na mienendo yao.

Advertisement Mabadiliko ya katiba

Mabadiliko ya katiba ya mwisho yaliwaondoa ujumbe wa Nec makatibu wa CCM wa mikoa waliokuwa wakiingia kwa nafasi zao na kuwaacha wenyeviti wa CCM wa mikoa kuendela kuwa wa-NEC.

Hata hivyo, taarifa za ndani za CCM zilisema kuondolewa kwa makatibu hao kumetengeneza udhaifu wa utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na Nec, kwa kuwa baadhi ya wenyeviti hawayafikishi kwa makatibu wao, huyafikisha kwa kuchelewa au kwa tafsiri isiyo sahihi.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, makatibu wa mikoa ambao ndio watendaji wa chama kwenye maeneo yao, mara kadhaa wameshindwa kutekeleza maagizo ya NEC na kudhoofisha shughuli za chama kwa kuwa hawakuyapata kwa usahihi au hayakufika kabisa.

Kuondolewa NEC

Chanzo chetu kilisema makatibu hao waliondolewa baada ya wajumbe wa NEC ya kumtafuta mgombea urais wa CCM iliyofanyika Septemba 21, 2015, kuimba “tuna imani na Lowassa” wakati Mwenyekiti wa CCM kwa wakati huo Jakaya Kikwete akiingia ukumbini.

Kipindi hicho kilikuwa cha mchakato ndani ya CCM wa kumtafuta mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na jina la Edward Lowassa lilikuwa limekatwa na vikao vya mwanzo.

Chanzo chetu kilisema makatibu wa mikoa wanahesabika ni watumishi wa chama, lakini kwa wakati huo hakuna aliyesimama kumtetea mwenyekiti kwa kuupinga wimbo huo.

Wa-NEC kupewa majukumu

Kwa mujibu wa chanzo chetu, wajumbe wa Nec hasa wa wanaowakilisha mikoa wamekuwa wakilalamika hawana majukumu ya kufanya baada ya vikao wanavyohudhuria vya Nec na kamati za siasa za mikoa yao.

Mabadiliko haya yanakwenda kuwapa majukumu wa-Nec kwa kuwanganisha na wajumbe wa mitaa ili waongeze nguvu kuratibu kazi za chama kwenye mashina ya maeneo yao.

Kofia mbili

Kwa mujibu wa chanzo chetu CCM inatarajia kurejesha mfumo wa uongozi wa kofia mbili kwa zile nafasi nyeti, ili wahusika waingie kwa nafasi zao.

Mfano, Rais anapochaguliwa kushika uongozi wa nchi vile vile awe mwenyekiti wa chama kwa nafasi yake badala ya kwenda kuchaguliwa tena ndani ya chama.

Hali ilivyo sasa, uchaguzi ndani ya CCM na ule wa nchi unafanyika tofauti, hivyo, kiongozi anayeondoka kwenye nafasi ya urais anabaki kuwa mwenyekiti wa chama hadi uchaguzi utakapofanyika mwaka mmoja baadaye.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, hiyo imekuwa ikiwalazimu wenyeviti hao kujiuzulu nyadhifa hizo ili kumpa nafasi aliye madarakani kuongoza Serikali na chama.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (marehemu) alijiuzulu uenyekiti wa chama na kumuachia Jakaya Kikwete aliyekuwa amechukua uongozi wa nchi na Kikwete alipoondoka madarakani alijiuzulu uenyekiti na kumuchia John Magufuli (marehemu).

Kwa mujibu wa chanzo chetu hilo linategemea na hiari ya mtu na wakati mwingine imekuwa ngumu katika utendaji wa kazi za Rais pale anapoingia kwenye vikao vya chama kama mwalikwa akisubiri muda wa uchaguzi.

Kauli ya Shaka

Katibu mwenezi wa CCM, Shaka alisema sababu ya kufanya marekebisho ya katiba ni kuongeza kasi ya ufanisi wa kazi za chama na utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya chama.

Shaka alisema pia lengo lingine ni kuongeza na kuimarisha udhibiti wa chama na viongozi wake wanaochaguliwa na kuongoza kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM kupiti Serikali za mitaa.

Mabadiliko yapunguza ajira

Mabadiliko hayo yaliondoka na ajira zaidi ya 170, hasa makatibu wasaidizi wa mikoa na wilaya na wenye vyeo visivyotambulika katika katiba waliokuwa wakilipwa mishahara, huku ikiondoa mzigo wa posho, ikielezwa kuwa kazi zao zitafanywa na makatibu wa jumuiya. Katika mlolongo huo, wamo makatibu wasaidizi wa mikoa ambao idadi yake ni 32 na wilaya 139, walipoteza ajira zao.

Mabadiliko mengine ni kupunguza wajumbe waliokuwa na kofia mbili kama vile wabunge na wajumbe wa Nec, isipokuwa tu pale ambapo wanalazimika kwa mujibu wa nafasi zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live