Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiza Mayeye ashinda Uenyekiti ACT-Wazalendo Kigoma

Act Mayeye.png Kiza Mayeye ashinda Uenyekiti ACT-Wazalendo Kigoma

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa zamani wa Viti Maalum, Kiza Mayeye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma.

Mayeye amepata nafasi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa kura 108 kati ya 134 za wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika mjini Kigoma Januari 13, 2024.

Katika kinyang'anyiro hicho, Mayeye amembwaga mshindani wake, Nicholous Cosmas aliyepata kura 24 huku Bailel Manwa akiambulia kura mbili.

Kabla ya kuhamia ACT-Wazalendo, Mwenyekiti huyo mpya alikuwa mwanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF) alikokuwa mbunge Viti Maalum na baadaye kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Sendwe Ibrahim amemtangaza Yunus Ruhonvya kuwa mshindi kwenye nafasi ya Katibu wa mkoa kwa kupata kura 65 ikiwa kura moja pekee dhidi ya kura 64 alizopata mshindani wake Frank Ruhasha.

Sendwe ndiye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma anayemaliza muda wake na kuamua kutogombea tena.

Nafasi ya Katibu Mwenezi imenyakuliwa na Azizi Ally kwa kuvuna kura za wajumbe 55 akimzidi kwa kura nne mshindani wake Kalembe Masoud aliyepata kura 51 huku mgombea mwingine, Feruzi akipata kura 25.

Tatu Amani ameibuka kidedea katika nafasi ya uenyekiti wa ngome ya wanawake baada ya kupata kura 14 na kumshinda Isabela Kabululu aliyeweka kibindoni kura mbili pekee.

Nafasi ya uenyekiti wa ngome ya wazee wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma imeenda kwa Selemani Simba huku Athumani Nyamitwe akiukwaa ukatibu wa ngome hiyo.

Ngome ya vijana wa chama hicho chenye uungwaji mkono mkoani Kigoma itaongozwa na Hamza Abdallah akiwa Mwenyekiti huku Katibu wake akiwa ni Uledi Amri Rajabu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live