Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitu wachambuzi wamesema kuhusu kauli za Rais Samia

SAMIA SULUHU12 Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu uwepo wa demokrasia, Katiba mpya, kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi na ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe vimewaibua Baadhi ya wachambuzi wa siasa, wasomi na viongozi wa vyama vya upinzani ambao wameonyesha kutofautiana naye.

Juzi yalirushwa hewani mahojiano ya Rais Samia na mtangazaji Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Salim Kikeke, ambapo Rais Samia alisema Serikali imetoa uhuru wa kidemokrasia kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa uhuru, lakini utawala wake haukubali siasa za fujo zinazofanywa kwa kivuli cha kudai Katiba mpya.

Katika mahojiano hayo Rais Samia alisema mahitaji ya wananchi kwa sasa si Katiba mpya bali huduma za maji, kilimo, afya na elimu lakini baadhi ya wanasiasa wa upinzani akiwemo Mbowe wanashikilia bango.

Alisema anatambua umuhimu wa Katiba mpya ni muhimu, lakini amewaomba Watanzania wampe muda wa kujenga uchumi na kuimarisha maisha ya mwananchi halafu baadaye ataugeukia mchakato wa Katiba mpya.

Wanasiasa, wadau na wasomi walisema Rais Samia hakupaswa kuzungumzia tuhuma zinazomkabili Mbowe kwa kuwa ameingilia mwenendo wa kesi inayoendelea kortini kwa sasa.

Pia, walisema kuwa Katiba mpya ni muhimu kwa kuwa huchochea uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa umma kwa wananchi na usimamizi mzuri wa rasilimali za Taifa.

Hata hivyo, Profesa Mohammed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema ni kweli wananchi wa hali ya chini wanahitaji kusikia zaidi mahitaji ya msingi ikiwemo maji, umeme lakini hawana elimu ya kutambua uhusiano uliopo kati ya Katiba na mahitaji hayo.

“Kundi la wachache werevu huibuka kuendesha madai ya kitaifa. Kuna kundi la asasi za kiraia, wanasiasa na vyombo vya habari, vuguvugu la kuingia mfumo wa vyama vingi waliokubali ni asilimia 20 tu lakini busara za Mwalimu Nyerere zikatumika,” alisema Profesa Bakari.

“Kwa hiyo ukisubiri wajitokeze wengi kudai Katiba matokeo yake huwa ni mabaya sana, mfano asilimia 80 ya Watanzania wajitokeze barabarani itakuwa vurugu na tishio kwa usalama wetu.”

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Dk Darius Mukiza, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), alisema uhuru wa vyombo vya habari chini ya Rais Samia haujaathirika.

Mwanasheria, Faraji Mangula alikiri kwamba kauli ya Rais Samia iliingilia uhuru wa mahakama kwa sababu alizungumzia kwa undani jambo ambalo tayari lipo katika mhimili huo.

“Kwa nchi zetu hizi, kauli ya Rais ni sheria, kwa hiyo itapeleka ujumbe kuwa suala hili lina baraka za Ikulu. Nadhani hakutakiwa kuzungumzia kesi ya Mbowe,” alisema wakili huyo wa kujitegemea.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus alisema katika suala la Mbowe, Rais alipotoshwa kwa sababu Mbowe alikuwepo nchini tangu Septemba, mwaka jana lakini hakukamatwa.

“Mbowe hakuondoka nchini baada ya uchaguzi, waliondoka akina Lissu (Tundu) na Lema (Godbless) lakini hakukamatwa kipindi chote hicho mpaka sasa lilipoibuka suala la katiba mpya, na ndipo hapo wakapata sababu za kumshitaki kwa kosa la mwaka jana,” alisema.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo za Chadema, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema aliyoyasema Rais Samia kwenye mahojiano hayo ndiyo kauli ya Serikali.

“Wao si wamesema, waache waendelee kusema huko. Rais jana amefanya interview na BBC, msikilizeni aliyoyasema Rais, ndiyo kauli ya Serikali, unataka kauli nyingine ya nini tena?” alisema Msigwa baada ya kutakiwa kufafanua kuhusu suala hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live