Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitu Zitto Kabwe kaongea kuhusu wanachama wa ACT Wazalendo

B4a41f3c9c363b90af5d07fdb7cece53 Kitu Zitto Kabwe kaongea kuhusu wanachama wa ACT Wazalendo

Mon, 1 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto amewataka viongozi wa chama hicho wa ngazi zote wakutane mara kwa mara na wanachama ili kukipa uhai chama hicho.

Zitto alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho.

Alisema uimara wa chama chochote cha siasa ni vikao katika ngazi zote kuanzia kata hadi taifa hivyo viongozi wa ACT Wazalendo wazingatie hilo ili pia kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

"Twendeni tukarejeshe hamasa ya wananchi wote vijijini, mitaani, katani, majimboni na mikoani kwa kufanya siasa za masuala yao, tuwe sauti yao, tuwe tegemeo lao , katika mazingira haya ambayo hayana tofauti na mazingira ya chama kimoja tunapaswa kuhangaika na watu" alisema Zitto.

Alipongeza utendaji kazi wa viongozi wa chama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman.

Zitto alisema kupitia serikali ya umoja wa mitaifa visiwani humo, chama hicho kimewezesha wahisani na mashirika ya kimataifa kutoa misaada na mikopo kwa kuwa kuna utulivu nchini humo.

Alisema chama hicho kimeandaa mpango maalumu wa kukiimarisha ili kutimiza wajibu kama chama cha upinzani kinachojiandaa kuongoza taifa.

"Kuanzia Januari mwakani, tutaanza rasmi mfumo huo ambao utabadili kabisa namna siasa zimekuwa zikiendeshwa nchini kwetu tangu mfumo wa vyama vingi uanze" alisema Zitto.

Alisema kwa sasa ACT Wazalendo kimemaliza kazi ya kuwatambua wanachama wake ambao watakuwa na majukumu maalumu na kuanzia mwezi huu chama hicho kitaanza kutoa mafunzo ili kutekeleza lengo hilo.

Awali Katibu Mkuu wa chama hicho,Ado Shaibu alisema kikao hicho cha kwanza cha Halmashauri Kuu ni utekelezaji wa katiba ya chama hicho inayotaka kukaa walau mara mbili kwa mwaka kujadili na kupeana miongozo kuhusu mambo ya chama hicho.

Chanzo: www.habarileo.co.tz