Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili uchaguzi atakayemrithi Lissu

65687 Pic+wema

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taarifa ya Spika, Job Ndugai kuwa Jimbo la Singida Mashariki lipo wazi na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea na utaratibu za uchaguzi, imeibua kitendawili cha nafasi hiyo kujazwa ndani ya muda uliotajwa kisheria kabla ya Bunge kuvunjwa.

Katiba ya Tanzania Ibara ya 90 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2015, kifungu cha 37 (6), zinaeleza kuwa uchaguzi mdogo utafanyika miezi 12 kabla ya Bunge kuvunjwa na Rais.

NEC hadi jana ilikuwa bado haijatangaza muda wa kampeni na siku ya kufanyika kwa uchaguzi huo na uhai kwa Bunge hili la Kumi na Moja unatarajiwa kukoma Julai au Agosti mwanzoni mwaka 2020 ili kupisha mchakato wa uchaguzi mkuu.

Kitendawili kilivyo

Kuanzia leo hadi Julai 31, zimebaki siku 27 kufikia siku hiyo ya mwisho ya uchaguzi mdogo au wa marudio.

Kitendawili kilichopo ni kama siku hizo 27 zilizobaki zitatosha kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo kwa kufuata mchakato uliowekwa.

Pia Soma

Kuanzia Agosti Mosi hadi Julai 30 mwakani ni siku 364 ambazo ni sawa na miezi 11 na siku 29 ambazo ni chini ya miezi 12 inayotajwa kisheria.

Chaguzi ndogo tatu zilizofanyika mwaka huu za ubunge zinaonyesha kuwa siku za kampeni pamoja na zile za uchukuaji na urejeshaji wa fomu na uteuzi wa wagombea ni zaidi ya siku 30.

Mathalani, uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki uliokuwa ufanyike Mei 19 baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Joshua Nassari kupoteza sifa za ubunge, mchakato wa uchukuaji fomu, urejeshaji na kampeni ilikuwa ni siku 31.

Ratiba iliyotolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage ilisema fomu za uteuzi wa wagombea zilitolewa kuanzia Machi 15 hadi Aprili 19, uteuzi wa wagombea ulifanyika Aprili 19. Kampeni za uchaguzi Aprili 20 hadi Mei 18.

Uchaguzi mdogo wa Ukerewe na Babati Mjini ulitumia siku 27 ambazo zilikuwa za kampeni na ukijiumulisha uchukuaji fomu na uteuzi zilikuwa siku 34. Pia katika uchaguzi mdogo wa Ukonga na Monduli, siku za kampeni zilikuwa 25, ukijumlisha siku za uchukuaji fomu na uteuzi zilizotolewa kuanzia Agosti 13 hadi 20 zilitimia siku 33.

Iwapo Bunge litavunjwa chini ya Julai 31 mwakani, kuna uwezekano jimbo hilo la Singida Mashariki ambalo lilikuwa likiongozwa na Lissu kuanzia mwaka 2010 hadi Julai 28, litakuwa wazi hadi mwakani.

Kauli ya NEC

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia akizungumza na Mwananchi kuhusu uhai wa Bunge na kufanyika kwa uchaguzi wa Singida Mashariki alisema uchaguzi utakoma baada ya miezi 12 kabla ya Bunge kuvunjwa.

Alisema baada ya Julai mwaka huu hakutakuwa na uchaguzi wowote utakaofanyika na kama itakuwa hivyo jimbo litabaki wazi hadi uchaguzi mkuu ujao mwakani lakini hilo litategemea na uamuzi wa Mahakama.

Alipoulizwa iwapo Agosti Mosi ikifika uchaguzi haujafanyika itakuwaje, Dk Kihamia alisema asingeweza kulizungumzia hilo hadi taarifa kwa umma itakapotolewa kuhusu taratibu za uchaguzi huo wa Singida Mashariki.

Kuhusu hilo, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema uchaguzi hauwezi kufanyika baada ya miezi 12 kabla ya Bunge kuvunjwa, “lakini kama kesi itaisha mapema kama ya Joshua Nassari kutokana na masuala ya kitaalamu, uchaguzi utafanyika.”

Alichokisema Lissu

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Lissu alisema, “hilo la uchaguzi kutokufanyika linawezekana kabisa.

Iwapo nitashinda kesi nitarudi bungeni, nikishindwa uchaguzi utafanyika lakini kama muda wa miezi 12 utakuwa umevuka, jimbo litakwenda wazi hadi mwaka 2020.”

Alipoulizwa mwenye haki ya kufungua kesi hiyo kati ya yeye (Lissu), wapigakura wake, familia yake au chama chake alisema ni yeye mwenyewe.

“Sheria inanitaka mimi mwenyewe au mwakilishi wangu mwenye mamlaka ya kusimamia masuala yangu ya kisheria. ‘mwakilishi mwenye mamlaka’ ni yule niliyempa mamlaka kwa maandishi, yaani ‘power of attorney,” alisema Lissu.

Akijibu swali lililotaka kujua huyo ‘mwakilishi mwenye mamlaka’ amekwisha kumpata na kesi hasa itafunguliwa lini, Lissu alisema “nikishampata mtasikia kwani haya mambo sio ya siri.”

Lissu amekuwa nje ya nchi baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2017 na tangu siku hiyo amekuwa nje ya nchi kwa matibabu yaliyotanguliwa na yale aliyoyapata katika Hospitali ya Rufaa Dodoma kisha Hospitali ya Nairobi Kenya na sasa Ubelgiji.

Juni 28, Spika Ndugai alitangaza bungeni kwamba Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutokujaza fomu za maadili ya viongozi wa umma pamoja na kutokutoa taarifa kwake (spika) ya wapi alipo hivyo kumhesabu kama mtoro bungeni.

Spika Ndugai alisema alimwandikia barua Mwenyekiti wa NEC kuhusu kiti hicho cha Lissu kuwa wazi na kumtaka kuendelea na utaratibu wa kujaza nafasi hiyo.

Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu alisema hakubaliani na hoja hizo za Spika Ndugai na atakwenda mahakamani kudai haki yake.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo ya Spika Ndugai alisema watakwenda mahakamani lakini wataanza kumwandikia barua Spika Ndugai ili awapatie uamuzi alioutoa bungeni.

Jana, Mwananchi lilitaka kujua kutoka kwa Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai iwapo barua hiyo imekwisha kufika na alisema, “binafsi sijaiona (barua).”

Chanzo: mwananchi.co.tz