Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili cha makatibu, Sumaye CCM

95359 Sumaye+pic Kitendawili cha makatibu, Sumaye CCM

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Frederick Sumaye amerejea CCM, makatibu wawili wa zamani, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana wameitikia wito, lakini matukio hayo mawili ni kitendawili wakati chama hicho kikijiweka sawa kwa uchaguzi mkuu.

Sumaye, ambaye siku 68 zilizopita kabla ya jana alijiengua Chadema akisema hatajiunga na chama chochote cha siasa isipokuwa kusaidia, jana alitangaza kurejea chama hicho akiwa amevalia shati lenye nakshi za rangi ya kijani, moja ya rangi mbili za chama hicho.

Baadaye mchana, CCM ikaeleza katika tovuti yake kuwa Kinana na Makamba, ambao kwa takriban siku tatu wamekuwa wakisemekana kukataa kuhojiwa, hasa na baadhi ya viongozi wachanga katika chama, wameitikia wito na baadaye katibu mkuu, Dk Bashiru Ali kuiambia Mwananchi kuwa wamehojiwa,

Kurejea kwao kunaweza kukawa kumeshusha pumzi kwa chama hicho ambacho kimekuwa kikikabiliana na migogoro kadhaa tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wakati Sumaye na waziri mkuu mwingine wa zamani, Edward Lowassa walipohamia Chadema pamoja na kundi la watu.

Jana Sumaye alitumia nafasi aliyopewa na Katibu Mkuu wa CCM. Dk Bashiru Ali kueleza sababu za kuchukua uamuzi unaotofautiana na ule wa mwaka 2015.

“Nimekuwa waziri mkuu kwa miaka 10 na kiongozi kwa miaka kadhaa. Nitakuwa sitendi haki endapo nitakaa mahali bila kutoa ushauri au mchango wangu kwenye Taifa,” alisema Sumaye huku akipigiwa makofi na wanachama.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Huwezi kutoa mchango kama hauna mahali na ukiutoa barabarani watu watakushambulia. Nikaona mimi si wa hadhi ya kufika kudharauliwa. Nikasema ngoja nirudi kwenye chama changu kilichonilea, kunikuza hadi nilipofika na kujivunia kuwa nina mchango katika Taifa hili.”

Huku mara kadhaa akisema CCM oyeee, Sumaye alisema amerudi ili aendelee kusaidiana na wanachama wenzake na wananchi wengine kukijenga chama hicho tawala nchini.

“Bila kuwapotezea muda nimeamua kurudi kwa sababu hii, matumaini niliyoyategemea ya kusaidia nchi tu, shida yangu ilikuwa ni nchi tu. Mimi nina uzalendo ambao huwezi kuutilia shaka na nilikuwa naangalia mbele sana kwa maslahi ya nchi, lakini imeshindikana,” alisema.

Pia aliwapiga vijembe wanasiasa wa upinzani.

Kutwanga maji

“Baada ya kuhangaika na hawa jamaa zangu, nikaona kwa kweli nabeba maji kwa gunia, Faida pekee ni kulowana mgongo tu,” alisema.

“Nimekuja huku tujenge chama chetu na nchi, kama kuna dosari za hapa na pale nitakuwa na sehemu ya kusemea na nitawashauri viongozi akiwamo katibu mkuu. Nikiwa ndani ya chama nina nafasi kubwa ya kutoa mchango wangu. Naomba mnipokee ndugu zangu.”

Wakati akiondoka CCM, alisema ameamua kujiunga upinzani ili auimarishe. Alisema nchi haiwezi kuwa na chama kimoja imara na vingine dhaifu na kwamba ni lazima kuwe na angalau chama kimoja imara cha upinzani ili kukitokea tukio lolote, kiweze kushika madaraka na kuongoza bila ya matatizo.

Lakini Dk Richard Mbunda anaona mambo ambayo Sumaye amethibitisha tabia ya baadhi ya wanasiasa kuangalia masilahi yao binafsi kuliko masilahi ya wananchi wanapofanya uamuzi wao.

“Zamani kulikuwa na wanasiasa kama vile (Waziri Mkuu wa India, Indira) Gandhi ambao walionekana kuwa tayari kufa kwa ajili ya wananchi wao. Lakini siku hizi wanaangalia masilahi binafsi. Ni mtu anayetafuta political relevance,” alisema.

“Tena amechelewa sana. Mimi nilitarajia angeondoka mapema tu wakati ule Lowassa anaondoka.”

Uchaguzi Kanda ya Pwani

Kauli hiyo inalingana na ya Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa, ambaye alihusisha hatua hiyo na kushindwa kwa Sumaye katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chadema ambako alikosa idadi ya kura za kutosha licha ya kugombea peke yake.

“Japo Sumaye alibaki upinzani baada ya makada wengi kuondoka, kule kushindwa kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Pwani kulimkatisha tamaa.”

Alisema Sumaye amejiunga katika msururu wa wanasiasa wanaoangalia masilahi binafsi.

“Wanasiasa wengi ni opportunists (wanaangalia fursa), si kuangalia masilahi ya wananchi na Taifa,” alisema.

“Akiona mambo yamebadilika anaondoka, akiona yamerudi naye anarudi. Unapokwenda upinzani uwe tayari kupambana na demokrasia au kama ni haki za binadamu unapambana.”

Lakini hatua hiyo ya Sumaye, mmoja wa wazungumzaji wakubwa katika kampeni za urais za upinzani 2015, imeibua kitendawili.

Ni nguvu hiyo ya ushawishi katika kampeni za 2015 ndiyo inamfanya arejeshwe CCM, ambako wakati anaondoka aliona haimthamini? Ni moja ya maswali yaliyoibuka mara baada ya kuonekana ofisi ndogo za CCM jana asubuhi.

Katika kipindi cha takriban miaka minne aliyokaa upinzani, amekumbana na migogoro na mamlaka za nchi, ikiwa ni pamoja na shamba lake la Mabwepande kuachiwa wananchi waliovamia.

Pia alipokonywa shamba lake la mkoani Morogoro kwa maelezo ya kutoliendeleza, na akalazimika kujiondoa bodi ya wakurugenzi ya benki ya CRDB kuepusha shari na mamlaka.

Suala hilo linaibua maswali kama uamuzi wake unaweza kuweka ukomo wa migogoro hiyo dhidi ya mamlaka.

Pia hatua hiyo inaibua utata kutokana na Sumaye kurudi CCM wakati kukiwa na habari za kuwepo kwa mzozo kati ya makatibu wakuu wa zamani na uongozi baada ya kuitwa kujieleza kuhusu sauti zilizosambaa mitandaoni zikihusishwa nao ambazo zilikuwa zikikisema vibaya chama hicho tawala, lakini habari nyingine zikidai wamekataa kuhojiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya maadili.

Kinana, Makamba waibuka

Jioni zilisambaa picha zinazowaonyesha Kinana na Makamba wakiwa katika ofisi pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama na maadili.

Kinana amekaa katika kiti kinachoangaliana na Phillip Mangula, ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo huku Dk Bashiru na wengine wakiwa pembeni.

Picha nyingine inamuonyesha Dk Bashiru akizungumza na Makamba katika dirisha la gari, lakini haionyeshi safari yake kwenda ofisini kama ilivyofanyika kwa Kinana.

Taarifa ya Humphrey Polepole, katibu wa uenezi wa CCM, ilisema jana kuwa makatibu hao walikubali kufika mbele ya kamati hiyo.

Wawili hao pamoja na Bernard Membe walitakiwa kuhojiwa makao makuu ya CCM, maarufu kama White House, lakini ni waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje pekee aliyeibuka jijini Dodoma kuhojiwa na kamati hiyo.

Habari zilienea kuwa waligoma kuhojiwa na walikitaka chama hicho kuamua mustakabali wao.

Wawili hao walishaanza maisha ya kustaafu, lakini hatua ya kuwahoji inaibua maswali kuhusu mustakabali wao.

Kinana, ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2012, anajulikana kwa kukitangaza chama hicho katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, akiwashtaki kwa wananchi mawaziri walioonekana kuwa mzigo.

Mara kadhaa kumekuwa na habari kuwa anatofautiana na uongozi na ndio maana alikuwa haibuki katika baadhi ya mikutano, hadi mwenyekiti wa CCM, John Magufuli alipolazimika kutoa ufafanuzi kuwa alikuwa mgonjwa na alimruhusu kwenda India kutibiwa.

Makamba, ambaye aliteuliwa mwaka 2007 kushika wadhifa huo, alishika wadhifa huo wa utendaji mkuu wa CCM wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na akabadilishwa mwaka 2011.

Wawili hao waliandika barua kwa uongozi wa kamati ya wazee wa CCM kulalamikia uongozi wa chama hicho kutowalinda dhidi ya watu wanaowachafua, wakimtaja mtu anayejiita kuwa mkereketwa wa Serikali ya Awamu ya Tano, ambaye walisema anaonekana kulindwa na mtu mwenye mamlaka.

Barua yao ilizagaa katika mitandao ya kijamii hadi pale sauti zao zilipoibuliwa mitandaoni, zikiwahusisha wawili hao pamoja na makada wengine watatu-- Membe, January Makamba, William Ngeleja na Nape Nnauye wakikizungumzia chama hicho kwamba kinapoteza mvuto.

Chanzo: mwananchi.co.tz