Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Kipimajoto’ cha Maalim Seif Ikulu ya Zanzibar

98320 Pic+maalim ‘Kipimajoto’ cha Maalim Seif Ikulu ya Zanzibar

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maalim Seif Sharif Hamad, mwanasiasa nguli aliyebaki maarufu katika miongo miwili katika siasa nchini na hasa Zanzibar, ameendelea kufungua mlango wa ikulu bila mafanikio, lakini safari hii anaapa iwe mvua liwe jua atashinda na kulinda ushindi wake.

Akiwa amegombea kiti cha urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, amedokeza kuwania kwa mara nyingine mwaka huu, iwapo atapatiwa ridhaa na chama chake cha ACT Wazalendo.

Kabla ya kujiunga na CUF, Maalim Seif aliwahi kutumikia nafasi ya Waziri Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 1984 hadi 1988.

Chini ya muafaka wa tatu wa Zanzibar, Seif aliteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), mwaka 2010-2015.

Machi 19, mwaka jana Maalim Seif aliwaongoza viongozi wenzake waandamizi 20, viongozi wa wilaya zote 11 za Zanzibar na wa majimbo 54 kujiunga na ACT-Wazalendo wakitokea CUF.

Pamoja na matumaini hayo, Dk Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) haoni matumaini makaubwa ya lengo la mwanasiasa huyo kufanikiwa kwa sasa, licha ya ushawishi, uwezo na uzoefu wa kiuongozi alionao.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Ukiangalia historia ya Maalim Seif na Zanzibar inasadikika kuna uchaguzi fulani aliwahi kushinda na mara kadhaa kuwa karibu sana na ushindi, ni mstahimilivu sana, lakini swali langu je, akishinda atatangazwa? Ni vigumu kwa sababu ni muhimu kurejea kwenye historia,” anasema Dk Mbunda.

Hali hiyo inamtuma Profesa Bakari Mohammed kutoka Idara hiyo pia anasema kuamini kuwa Maalim Seif sasa anastahili apumzike tu kutokana na mazingira yaliyopo.

Anasema ni vema akabakia kuwa mshauri wa masuala ya siasa na kujengea uwezo kwenye chama chake.

“Kutokana na umri wake pamoja na hali ya kisiasa visiwani humo, ingekuwa busara akapumzika awaachie vijana, wafuasi wanaweza kuwa wanamtaka yeye lakini inabidi kuangalia hali ilivyo. “Hii itamsaidia kulinda heshima yake kwa sababu hakuna dalili za kushinda na kutangazwa mshindi wa urais,” anasema Bakari.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi juzi Maalim Seif alisema hana mpango wa kustaafu siasa wala kuacha kugombea nafasi ya urais kwa sababu anachoangalia yeye hivi sasa ni kuungwa mkono na wananchi.

“Mimi ni mwanasiasa, ninaloangalia kubwa ni imani ya wananchi kwangu. Mara zote nilizogombea niliamini wananchi wana imani na mimi, ndiyo maana ninashinda,” alisema. Anasema hata uchaguzi wa mwaka huu, tayari kuna watu wameshaanza

kumshawishi agombee urais, wanasubiri uamuzi wake. “Kwa hiyo nasema, Abdoulaye Wade (rais mstaafu wa Senegal) aligombea mara ngapi? Hatimaye si alishinda na akatangazwa?” alisema.

“Wakati wowote nitakapoona napoteza imani ya wananchi basi sitaendelea. Lakini kwa sasa bado wana imani na mimi, CCM wanajua mwaka 2015 tuliwazidi kura.”

Lakini akizungumzia hilo, Profesa Bakari anasema haoni dalili zozote za Ikulu ya Zanzibar kuwa chini ya chama cha upinzani kwa sasa. “Hofu naona bado iko kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwamba unaweza kutetereka nje ya CCM. Kwa hiyo Maalim Seif alinde heshima yake, apumzike tu.”

Tofauti na mawazo hayo ya msomi huyo, mwenzake Profesa Mohammed Makame Haji wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Zanzibar anasema anaamini upinzani unaweza kuongoza Zanzibar hata kwa kipindi hiki endapo wapiga kura wataamua. “Ushindani ni mkubwa, ila tatizo siasa za CCM, CUF zinatawaliwa na historia. Wapiga kura hawaangalii sera au ilani, ni makundi ya kihistoria yaliyotengenezwa na vyama huku Zanzibar. Mfano kundi la waliohamia ACT kutoka CUF ni la kihistoria, kwa hivyo viongozi wamalize hili tatizo,” anasema Profesa Haji.

Maoni ya Profesa Haji yanaungwa mkono na Kaimu katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akielezea jinsi chama hicho kilivyojipanga kushinda. Anasema kimejenga misingi na idadi ya wanachama inaongezeka.

Hata hivyo, anasema suala hilo linategemea uvumilivu wa kisiasa kwa Serikali iliyopo madarakani. Katika eneo la uvumilivu, Semu hayuko mbali na wanasiasa wengine wanaotamani iwepo Tume huru ya uchaguzi ili kuweka uwanja sawa wa kisiasa, suala ambalo hata kila upande unalitazama kwa mlengo wake.

2020 itakuwaje?

Katika mahojiano na Mwananchi siku chache zilizopita, Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema ahadi ya uchaguzi huru na haki inatekelezeka.

Anasema hata Rais wa Zanzibar na Dk Ali Mohamed Shein angetamani kuona uchaguzi huru na haki ukifanyika Oktoba mwaka huu.

“Wakati anamaliza kujiandikisha kwenye Daftari la Mzanzibari Mkaazi, Dk Shein alisema anaondoka, kwa hiyo angependa pia anayemrithi apatikane kutokana na uchaguzi ulio huru na haki.

“Chama (CCM) pia kupitia halmashauri kuu kitasimamia utekelezaji wake, sasa mashaka ni mengi kwa wanasiasa, uzuri uliopo hata uchaguzi mkuu Mahakama Kuu pia inahusika. Ushahidi upo kwa hiyo (wapinzani) wafuate sheria.”

Kuhusu madai ya CCM kutokuwa tayari kukabidhi madaraka kwa Maalim Seif kwa sasa hata kama atashinda, Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Mabodi anaomba kutoa ufafanuzi wa swali hili kwa mahojiano maalumu.

Hata hivyo, Maalim Seif anasema anaamini uchaguzi huo ataishinda CCM kutokana na hesabu alizofanya na kwamba hatakubali kuona wapiga kura wakipokonywa ushindi wao.

“2020 CCM tutaishinda vibaya sana na tukishinda tutalinda ushindi wetu, hatutakubali tena, ni wajibu wa kila chama na Serikali kuheshimu uamuzi wa wananchi. Siyo kikundi kiamue kumweka rais wanayemtaka madarakani, waliofanya hivyo sasa mwisho, huo ndiyo msimamo wangu.”

Safari ilianzia wapi?

Safari ya Maalim Seif kugombea urais ilianza mwaka 1995 akichuana na mgombea wa CCM, Salmin Amour. Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo, CUF ilitangaza kutoutambua ushindi huo.

Mwaka 2000, Maalim Seif aliingia ulingoni kupambana na Amani Abeid Karume, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. Matokeo ya ZEC yalionyesha Seif alijikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume.

Majeraha ya uchaguzi huo yalijitokeza zaidi mwaka 2001, baada ya wafuasi wa CUF kuuawa katika maandamano ya Januari 27, 2001. Maandamano hayo yalichangia kusainiwa kwa makubaliano ya pili ya amani baina ya CUF na CCM ili kuleta utulivu visiwani Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka 2005, CUF ilimteua Maalim Seif kupambana tena na Amani Abeid Karume wa CCM. Uchaguzi huo ulipokamilika, ZEC ilimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada kujikusanyia asilimia 53.18, huku Seif Hamad akijipatia asilimia 46.07 ya kura zote.

Hata hivyo, waangalizi wa kimataifa walidai uchaguzi huo haukuwa huru na haki. Taarifa ya waangalizi wa Jumuiya ya Madola walisema palikuwa na kasoro nyingi na ukosefu wa uhuru, miongoni mwa wapigakura na wagombea. Katika matokeo hayo, CUF ilipinga matokeo hayo. Maalim Seif alirudi tena kwenye kinyang’anyiro cha mwaka 2010 akiwakilisha CUF dhidi ya Dk Ali Mohammed Shein wa CCM. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 31, 2010, ZEC ilimtangaza Dk Shein kuwa mshindi wa urais Zanzibar kwa kupata asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za Maalim Seif.

Muafaka ulikwama wapi?

Jjitihada za usuluhishi zilianza kwa muwafaka wa mwanzo kusainiwa Juni 9, 1999 baina ya CCM na CUF ili kufanya mazungumzo ya kutatua hali iliyojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa 1995.

Kamati ya Pamoja ya CCM na CUF yenye Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 14 ilifanya mazungumzo chini ya usuluhishi wa Jumuiya ya Madola na baadaye Julai 2000 iliwasilisha ripoti serikalini, iliyoandaa na kupeleka mswaada maboresho ya katiba katika baraza la wawakilishi lakini CUF walikataa kwa madai ya hujuma na muafaka wa kwanza ukazima.

Muwafaka wa pili Oktoba 10, 2001, ulichagiza kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Rais ya kusimamia utekelezaji wa muafaka wa baina ya vyama hivyo hatua iliyofanikisha marekebisho ya Katiba ya Zanzibar 2002/03 lakini suala la serikali ya umoja wa kitaifa halikuingizwa.

Hata hivyo, muafaka mwingine uliozaa SUK ulikwama mwaka 2015 na Profesa Mohammed Makame Haji wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Zanzibar anasema marudio ya uchaguzi wa mwaka 2015 ndiyo sababu ya mkwamo huo.

“Ukiangalia serikali ingeweza kutumia nguvu zake lakini ilionyesha nia ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ikakubali muafaka huo, kama CUF walijua wana wafuasi wengi basi wangereja marudio ili kuunda serikali hiyo, haikuwa na sababu kususia,” anasema Profesa Haji.

Chanzo: mwananchi.co.tz