Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiongozi Chadema mbaroni akidaiwa kumshambulia mtendaji

83077 Pic+tarime Kiongozi Chadema mbaroni akidaiwa kumshambulia mtendaji

Fri, 8 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Huku kukiwa na taarifa za wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa katika vijiji na mitaa kadhaa za halmashauri ya Tarime vijijini na Tarime mji, Jeshi la Polisi linamshikilia kigogo wa Chadema wilayani humo kwa madai ya kumpiga mmoja wa watendaji wa kata.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumanne Novemba 5, 2019, Katibu wa Chadema mkoa wa Mara, Chacha Heche amemtaja kiongozi anayeshikiliwa kuwa ni Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Wilaya ya Tarime, Sabato Amos.

“Askari Polisi waliomkamata katibu wetu wa Bavicha pia wametueleza kuwa wanawatafuta viongozi wetu wengine wawili kwa madai kuwa kuna mtendaji wa kata ambaye hawajamtaja jina wala kata yake amefungulia kesi ya kushambuliwa na viongozi hao,” amesema Heche

 Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema taarifa za kushikiliwa kwa kiongozi huyo wa Chadema hazijamfikia na kuahidi kufuatilia.

 “Polisi tulipata taarifa ya kuwepo mkusanyiko wa watu katika ofisi za Chadema wilaya ya Tarime na vijana wangu walienda huko kufuatilia; sijapata taarifa kama kuna anayeshikiliwa. Ngoja nifuatilie nitakujulisha,” amesema Kamanda Mwaibambe

Wakati Kamanda Mwaibambe akisema hana taarifa za kukamatwa wala kusakwa kwa viongozi wa Chadema, Katibu wa chama hicho mkoa wa Mara, Heche Chacha amewataja viongozi wengine wa Chadema wanaosakwa na polisi kuwa ni Katibu Mwenezi wa wilaya ya Tarime, Pamba Chacha na Hamisi Nyansu ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri Tarime mji. Kuhusu watu kukusanyika ofisi za chama hicho kikuu cha upinzani mjini Tarime, Heche amesema waliokuwa eneo hilo ni viongozi na wagombea ambao majina yao yamekatwa katika mchakato wa uteuzi waliokuwa wakijadiliana hatua za kuchukua fomu na ya kukata rufaa.

Kuhusu hali ya ulinzi na usalama, Kamanda Mwaibambe amesema hadi saa 8:00 mchana, hakukuwa na taarifa yoyote ya uvunjifu wa amani na askari wa jeshi hilo wamesambaa maeneo mbalimbali kufuatilia matukio yanayoendelea katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaoendelea.

Usuli:

Kigogo mmoja wa Chedema anashikiliwa na polisi wilayani Tarime huku wengine wawili wakisakwa kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la kushambuliwa kwa mtendaji wa kata ambaye jina wala kata yake haijajulikana anayedaiwa kufungua kesi polisi.

Chanzo: mwananchi.co.tz