Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinana rasmi uenyekiti TCD

9e0e73375236039f167a97fd4b2b6766 Kinana anachukua uongozi kutoka kwa Zitto Kabwe

Thu, 7 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makam Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amekabidhiwa uenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Kinana amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACTWazalendo, Kabwe Zitto ambaye muda wake wa uongozi umekwisha.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Katiba ya TCD jana katika makabidhiano hayo jijini hapa, Kinana alisema amekuwa ni mtu wa bahati.

“Siku tano zimekuwa za bahati kwangu, napata cheo kimoja hadi kingine, mkipata muda mje niwaambie mganga wangu ni nani,” alisema Kinana ambaye Jumamosi iliyopita alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara.

Aliahidi kujitahidi kutimiza wajibu wake na matakwa ya Katiba. Aidha, kituo hicho kimeandaa mpango mkakati wake kuanzia mwaka 2022- 2026. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TCD, Bernadetha Kafuko, nafasi ya Mwenyekiti hudumu kwa muda wa miezi sita.

Kafuko alisema kituo hicho kilifanya uchaguzi wa kukabidhiana madaraka na huwa hawapigi kura.

Alisema nafasi ya Mwenyekiti ilikuwa ikishikiliwa na Zitto na baada ya muda wake kuisha nafasi hiyo itashikiliwa na CCM kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake atatoka Chama cha Wananchi (CUF).

Zitto alikabidhiwa cheti cha pongezi kutambua mchango wake katika nafasi ya uenyekiti wa TCD.

“Kwa kipindi cha miezi sita Zitto amefanya kazi nzuri sana, tulijiuliza zawadi gani nzuri ya kumpa tukasema tumpatie cheti cha pongezi,” alisema mtendaji huyo.

Katika mkutano wa TCD juzi, Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi alisema serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya siasa kwani Tanzania haijengwi na mtu mmoja wala chama kimoja, wote kama Watanzania lazima wajadili kwa umoja.

“Tukikubaliana jambo tutekeleze wote kama Watanzania, atakayekiuka ni mkosaji kwani atakuwa ameenda kinyume na makubaliano,” alisema Rais Samia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live