Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinana ataka viongozi wakosolewe kwa utaratibu

Kinana Bukombe Kinana ataka viongozi wakosolewe kwa utaratibu

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM -Bara), Abdulrahman Kinana, ametaka viongozi na watendaji serikalini kuzingatia kanuni, sheria, utaratibu na Katiba wanapowakosoa watendaji.

Amesema ni vyema wakajifunza kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pamoja na kuwa na uwezo na mamlaka lakini hajawahi kusimama hadharani na kuvunja haki ya utu wa mtu, hususani watendaji katika ngazi mbalimbali.

Kinana amesema hayo leo Desemba 13, 2023 akiwa Ushirombo, wilayani Bukombe, mkoani Geita alipozungumza na wanachama wa CCM, viongozi na wananchi kwenye tukio la kuzindua jengo la ofisi za chama hicho ngazi ya wilaya.

“Nataka kufafanua hili ambalo nimezungumza katika mkutano mkuu hapa Bukombe, ni kwamba viongozi wanaowasimamia watendaji serikalini, wasimamie sheria, kanuni na utaratibu lakini si vizuri kuwasema hadharani na kuwafedhehesha watendaji wa Serikali,” amesema.

Kinana amesema, “Mfano mzuri wa kuigwa ni wa Rais Samia Suluhu Hassan kwani hatujawahi kuona akisimama hadharani akimfedhehesha mtendaji serikalini, kwa sababu yeye ni muumini wa utawala bora unaozingatia Katiba, sheria, kanuni na utaratibu.”

Kinana amesisitiza watendaji wote wa Serikali kusimamiwa na kanuni, sheria, Katiba na utendaji serikalini.

Amesema watendaji hao wanasimamiwa na tume mbalimbali zinazosimamia maadili ya utendaji na nidhamu serikalini, hivyo ni vizuri kutumia utaratibu huo.

“Ninyi wenyewe mmeona mfano mzuri wa Rais, tuige huu mfano. Rais hajawahi kusimama hadharani hata siku moja akamfukuza mtumishi kazi kwa kuwa anaelewa utararibu na anauzingatia, tunawataka viongozi na watendaji serikalini kuzingatia hilo.

Amesema, “Mfano mwingine naweza nikawapa, kuna ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kuzingatia ripoti ya CAG, Rais ana uwezo wa kumfukuza mtu yeyote wakati wowote kwa sababu anazozijua yeye.

Kwa mujibu wa Kinana, Rais Samia hafanyi hivyo bali husubiri utaratibu na kanuni zifuatwe kwa sababu anaweza kumfukuza au kumsema mtu hadharani, baadaye ikabainika hana kosa, “Sasa unamuombaje radhi.

Amewataka viongozi kuurudisha utaratibu wa kuzingatia utawala bora, kuheshimu sheria, kwa kuwa hata Katiba inasema utu wa mtu ni lazima uheshimiwe.

Kinana amempongeza mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko, ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa kubuni na kuleta mawazo ya ujenzi wa ofisi.

Amesema mawazo hayo yalienda kamati ya siasa na Halmashauri Kuu na baadaye kwa wanachama, hivyo uamuzi wa kujenga majengo hayo ukafanyika.

Kutokana na kufurahishwa na ujenzi huo, Kinana ameitaka CCM Mkoa wa Dar es Salaam kujenga ofisi za kisasa za wilaya zake kama ilivyo Bukombe.

Amesema wanaCCM nchi nzima wana wajibu wa kuhakikisha ofisi wanazojenga na kumbi zinafanana na heshima na hadhi ya ukubwa wa chama hicho.

Kwa upande wake, Dk Biteko amemshukuru Kinana kwa heshima aliyowapa CCM Bukombe ya kuzindua majengo ya ofisi.

Amesema wadau wamechangia ujenzi wa majengo hayo, wakiwamo wanaCCM wenyewe ndani ya Wilaya ya Bukombe hasa vijana walioshiriki shughuli za ujenzi kwa kujitolea, wananchi wa makundi mbalimbali, baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali. 

Amesema mradi unaofuata utahusisha makazi ya watumishi wa CCM, wakiwamo makatibu wa chama hicho ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.

Naye, Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa ofisi hizo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amesema uzinduzi wa majengo hayo ni awamu ya pili.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalikwa amesema uongozi wa chama hicho wilayani humo umekuwa ukitumia njia ya vikao, kanuni na taratibu kuwasimamia watendaji wa Serikali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live