Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana amemsafishia njia Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa baada ya kuwaambia wanaoataka kuwania kiti hicho ndani ya CCM wajitafakari watafanya nini zaidi ya aliyoyafanya mbunge wa sasa jimboni humo.
Hata hivyo, Kinana aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, amesema moja ya sifa ya chama hicho tawala ni demokrasia, akisema mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote.
“Niwasihi wananchi wa Rufiji moja ya sifa ya chama chetu ni demokrasia, kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote, lakini ningependa kabla ya hujagombea ubunge wa Rufiji kwa kuangalia yaliyofanywa na Mchengerwa jiulize je, unaweza kufanya nini zaidi kuliko alichokifanya Mohamed.
“Jiulize tu, niliwahi kusema kule Kibiti, viongozi hawabadilishwi kama mashati, ukikaa naye muda ni vizuri, lakini kila baada ya miaka mitano ukibadilisha maana yake mnakuwa na wanafunzi. Haki ya kugombea anayo kila mtu, lakini ni vizuri mliye naye anafanya kazi? Ndio anawasikiliza ndio mnabaki naye ili mwende mbele pamoja,” amesema Kinana.
Kinana ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 30, 2023 wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu na mabalozi wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Katika mkutano ambao ulikuwa unalenga pia kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofanyika ndani ya miaka miwili jimboni humo.
Pia, katika mkutano huo, Kinana alikabidhi pikipiki 57 kati hizo 52 zinapelekwa katika kata 13 za jimbo hilo kwa mgawanyo wa bodaboda nne, huku ofisi ya Wilaya ya Rufiji ikipewa tano.
Mbali hilo, Kinana alikabidhi baiskeli 110 kwa ajili ya makatibu wa matawi wa CCM wilayani humo.
Kinana ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mchengerwa kwa kazi nzuri anayoifanya katika jimbo lake, ikiwemo kutoa vitendea kazi kwa CCM na jumuiya zake, akisema Rufiji imebadilika tofauti na miaka iliyopita.
Awali Mchengerwa amesema ndani ya miaka miwili na nusu mambo yamebadilika katika jimbo hilo, hasa sekta za afya akisema karibu kila kata za wilaya hiyo zimejengwa vituo vya afya ili kusogeza huduma kwa wananchi.
“Mpango uliopo hivi sasa ni kumaliza changamoto za afya katika kata zilizobaki ikiwemo Ngwala na tutajenga hospitali ya kisasa itakayogharimu Sh10 bilioni.
“Katika vituo vilivyojengwa Rufiji na maeneo mengine tutahakikisha madaktari na watoa huduma za afya watakaoajiriwa wanapelekwa huko. Baada ya ujenzi kukamilika kazi kubwa inayofuata ni Serikali kutoa ajira na imeshatoa kibali katika sekta hii,” amesema Mchengerwa.
Kuhusu miundombinu, Mchengerwa amesema kilikuwa kilio cha wananchi wa Rufiji kwa miaka mingi hasa eneo korofi la Nyamwage hadi Utete, lililowang’oa wabunge wengi na kusababisha Rufiji kuwa jimbo linalokaliwa kwa muhula mmoja.
“Mvua ikinyesha wananchi wa Rufiji wanatumia muda mrefu kwenda kupata huduma katika makao makuu ya wilaya Utete, nikutaarifa Makamu Mwenyekiti (Kinana), Serikali imeshamlipa mkandarasi fedha za ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyamwage hadi Utete kilomita 33.7,” amesema Mchengerwa.
Amesema tayari Serikali imeshasaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara utakaofanyika kwa miezi 18 na watahakikisha wanaweka taa za barabarani.