Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kukusanya mapato mengi na kuyatumia kwa faida ya wananchi kwa kujenga miradi ya maendeleo.
Akizungumza jana Julai 25, 2022 na wananchi wa Kata ya Itenka katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo Cha Afya Itenka, Kinana ameelezea hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuleta maendeleo ya wananchi huku akieleza kuwepo kwa mapato mengi kumechochea maendeleo.
“Serikali imeendelea kukusanya mapato na kutumia mapato kwa faida ya wananchi, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Serikali imepanga mipango yake ya maendeleo na hadi leo hapa Nsimbo kuna miradi mingi kama ilivyoorodheshwa, kila eneo limeguswa ujenzi wa barabara kuu, barabara za vijijini na zahanati, hospitali ujenzi unaendelea.
“Kuna hospital ya Rufaa kupitia Mkoa tayari inajengwa, umeme unasambazwa, mkoa mzima umeme umebakia vijiji saba na mwaka huu hivyo vijiji Saba navyo vitapata umeme, nimeambiwa kuna tatizo la umeme ambao unakatikakatika na unakatika kwa sababu unatumia jenereta. Sasa kazi imeanza ya kutengeneza utaratibu ili umeme unaokuja uwe wa Grid ya Taifa, umeme utoke Tabora na kuja moja kwa moja mpaka Katavi,” amesema Kinana.
Ameongeza kuwa mwaka ujao wakati kama huu mradi huo wa umeme utakuwa umekamilika kwani Katavi itakuwa imejiunga na gridi ya Taifa, hivyo umeme hautakatika tena. “Naomba muwe wavumilivu na mvumilivu hula mbivu baada ya muda mfupi tutachukua haya majenereta na kuyapeleka kwenye maeneo mengine kabisa” .
Aidha Kinana amesema katika Mkoa wa Katavi kuna barabara za lami zinaendelea kujengwa kwa kuunganisha Mkoa huo na mingine na anahakika mpaka mwaka ujao barabara hizo zitakuwa zimekamilika.
Kinana pia amewapongeza Wananchi wa Itenka na hasa Nsimbo kwa juhudi wanazofanya za kujitegemea na wamekuwa wakulima wazuri wa mpunga.”Mnafanya kazi kubwa ya kuzalisha mpunga na sasa hivi naambiwa bei yake imekwenda juu ,Kuna mtu anawapangia bei?Anayepanga bei ni nani? Ni anayetoa jasho akalima
“Lakini kuna jambo lingine nataka niseme hapa ndugu Mkurugenzi kwanza nikupongeze kwa kazi nzuri unayofanya na watendaji wenzako chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya kwani mnafanya kazi nzuri, hamuonekani,mnafanya kazi nzuri,hamsimami kwenye majukwaa ,hamsifiwi, mara nyingi mnalaumiwa sasa mimi nataka niwasifu kwa kazi nzuri mnayofanya.
“Ila kuna taratibu ,mkulima hatakiwi kutozwa ushuru wakati anaisafirisha lakini kuna malalamiko ya baadhi ya wakulima wanalalamika kutozwa ushuru.Mkurugenzi nadhani tulikubaliana kuna sheria watu wameziacha ,wanatengeneza sheria zao ,ukiwa na tani moja hakuna kusimamishwa kwani Kwa mujibu wa sheria tani moja haitozwi ushuru,”amesema Kinana.
Amefafanua isije kukawa na kuna watu wanakwenda kusimamisha wakulima wanajifanya wao ndio Serikali.”Anasimamishwa mkulima anaambiwa simama, toa ushuru,unamwambia nina tani moja unamwambia hapana,ukiuliza kwanini kwasababu ananguvu ya Serikali.Hiyo Serikali ni ya nani ? Si ya wananchi? Kwa hiyo wenye kauli ni wananchi.
“Sasa nataka niseme hivi tuelewane watakaondoa umasikini wa wananchi ni wananchi wenyewe kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ya watu kuondokana na umasikini, tusiwasumbue wananchi,tusiwawekee vikwazo ,tusiwawekee vigingi vingi ,tusiwatoze ushuru mwiingi, kila hatua ushuru,kila hatua ushuru ndio maana muuliza karanga anazunguka kwasababu hana kituo huwezi kumtosha ushuru”.
Kinana amesisitiza Serikali inapozungumza habari ya sekta binafsi,basi sekta binafsi wa kwanza ni mwananchi wa kawaida anayetafuta maisha yake kwa kulima,kwa kufanya biashara ndogo ndogo ,kuuza mifugo,duka,nyama na kwamba Mwananchi huyu anachotaka asisumbuliwe na Serikali.
“Na kazi ya madiwani ni kupunguza kero kwa wananchi, sisemi msitunge sheria za kodi tungeni sheria lakini sheria zisiwe mpaka mtu unashindwa kupumua.Rahisisheni maisha ya wananchi , kazi ya Serikali kujenga vituo vya afya,kuweka maji, umeme, kutengeneza Barabara kwa Vijijini na barabara Kuu.”