Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kina Polepole mikononi mwa Samia

GWAJERRYPOLE Kina Polepole mikononi mwa Samia

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunge watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, Josephat Gwajima na Jerry Silaa watajieleza mbele ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na tuhuma dhidi ya ukosefu wa maadili ndani ya chama.

Wabunge hao wanaotuhumiwa kukiuka maadili ya chama, walianza kujieleza kwenye vikao tofauti ikiwamo kwenye kikao cha kamati ya maadili ya wabunge wa CCM.

Baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, taarifa iliwasilishwa mbele ya Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa hatua.

Pia, Gwajima na Silaa waliitwa kujieleza mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Silaa anashtakiwa kwa madai ya kusema uongo kuhusu mishahara ya wabunge kutokukatwa kodi jambo aliloshindwa kulithibitisha wakati Askofu Gwajima anashtakiwa kwa kinachodaiwa kuleta taharuki.

Gwajima alidaiwa kusema uongo kuhusu viongozi kupewa hongo ili waruhusu chanjo ya Uviko- 19 huku Polepole akitajwa kushabikia mambo hayo kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alisema kuitwa kwa wabunge hao kunatokana na agizo la Kamati Kuu ya CCM iliyoketi jijini hapa juzi.

Shaka alisema Kamati Kuu ilijadili kuhusu wabunge hao baada ya kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 2017, kamati hiyo ya usalama na maadili ipo chini ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, mbali ya kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Samia, katibu wa kamati hiyo ni Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo. Wajumbe wa kamati hiyo ni makamu wawili wa mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula (Bara) na Dk Ali Mohamed Shein(Zanzibar).

Wajumbe wengine ni Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, manaibu katibu wakuu wa CCM, Dk Abdallah Juma Mabodi (Zanzibar), Christina Mndeme (Bara), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wajumbe wanne wengine wa kamati kuu, wawili kutoka Bara na wawili Zanzibar.

Shaka alisema baada ya kamati hiyo kukutana ilipeleka taarifa yake kwenye Kamati Kuu iliyoagiza wabunge hao waitwe kujieleza kutokana na dosari na mienendo yao.

“CCM ina Katiba, kanuni na taratibu, mtu akikengeuka chama kinarudi kwenye misingi yake kwa kuwaita na kuwahoji,” alisema Shaka.

Alisema wabunge hao wataitwa wakati wowote. “Kwa sasa ni kupanga kikao na kuwajulisha,” alisema.

Shaka alisema wabunge waliohijiwa na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM ripoti yake iliwasilishwa kwenye chama na uamuzi wanaitwa kwa ajili ya kujieleza.

“Chama kimepokea taarifa ya viongozi wake kukiuka maadili, wataitwa kwa mujibu wa taratibu za chama. Tarehe ya kuwaita itapangwa ikiwamo kuwajulisha wahusika,” alisema Shaka.

Gwajima na Silaa itakuwa mara ya tano katika makosa hayohayo kuwa wamekwenda mbele ya kamati tatu tofauti, lakini tayari walishahukumiwa na Bunge kwa kufungiwa mikutano miwili na kulipwa nusu mshahara.

Polepole itakuwa mara yake ya tatu kufika mbele ya kamati, lakini juzi aliitwa mbele ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wamekifungia kwa muda usiojulikana kipindi cha Shule ya Uongozi kinachomilikiwa na mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais kwa makosa matatu likiwemo la kutoa taarifa ya upotoshaji kuhusu chanjo ya Uviko-19.

Kuhojiwa Bungeni

Pia, wabunge Gwajima na Silaa walihojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge waliyokuwa wajumbe na waliondolewa ujumbe wa kamati.

Pia, Spika Job Ndugai aliwahamisha wabunge wanne kutoka kamati za awali kwenda kamati zingine huku maswali yakiwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, Humphrey Polepole ambaye amepelekwa kamati ya Sheria ndogo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live