Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio cha maridhiano ya CCM, wapinzani kinavyoshika kasi

90616 Maridhiano+pic Kilio cha maridhiano ya CCM, wapinzani kinavyoshika kasi

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilio kipya cha vyama vya upinzani nchini ni kuwapo kwa maridhiano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Kilio hicho kimetolewa miezi michache baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ulisusiwa na vyama vinane vya upinzani kwa madai ya kuwapo kwa figisu nyingi pamoja na wagombea wao wengi kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.

Wakati vyama vya upinzani vikitoa kauli hiyo, hivi karibuni wadau wa siasa, viongozi wa dini na wanaharakati walihimiza kuwapo kwa maridhiano kutokana na matukio mbalimbali ya kisiasa yanayoendelea nchini.

Hali hiyo inachangiwa zaidi na mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2015. Kwa zaidi ya miaka minne sasa, vyama vya siasa hasa vya upinzani vimekuwa katika mazingira magumu ya kufanya siasa baada ya Rais John Magufuli kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano mpaka 2020.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama chake kimejiimarisha zaidi katika ngazi za chini na kupata wanachama wengi.

Pamoja na hayo, Chadema na vyama vingine vinaona bado kuna umuhimu wa kuwapo kwa maridhiano kuelekea uchaguzi mkuu ili kuweka mazingira mazuri ya kushiriki uchaguzi.

Desemba 9 mwaka jana, Mbowe akiwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika jijini Mwanza, alitoa kilio hicho mbele ya Rais Magufuli kwa kueleza kuwapo kwa ulazima wa maridhiano, upendo na mshikamano nchini.

Alisema Rais Magufuli ana nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano hayo, kwani kuna wengine wanalalamika wanaumia.

Kauli ya Mbowe iliungwa mkono juzi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliyemwomba Rais Magufuli kukutana na vyama vya siasa ili kuweka mazingira mazuri ya kushiriki uchaguzi wa 2020.

Lipumba alisema ni vema Rais Magufuli akakutana na viongozi hao ili kujadiliana na kuzungumza masuala mbalimbali yatakayosaidia kuepusha yaliyojitokeza katika uchaguzi wa Serikali za mitaa. Hata hivyo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema chama hicho kimekuwa kinahitaji maridhiano na ushuhuda upo kupitia kwa viongozi wake, lakini lazima kuwepo na muktadha sahihi.

Anatoa mfano kuwa baada ya maridhiano ya Zanzibar kati ya CCM na CUF kulifanyika uchaguzi wa amani na kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa ilipata mafanikio makubwa, kwani wakulima wa karafuu walipata bei nzuri lakini tangu serikali hiyo ilipoanguka, hali imerudi kama ilivyokuwa zamani.

“Kuna faida kubwa ya maridhiano, sisi kama chama hatupingi, bali suala tulilokuwa na mashaka nalo ni muktadha. Tumetoka katika uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao mchakato mzima wa uchaguzi umechukuliwa, umeporwa. Wananchi wameporwa haki yao ya kuchagua na ya kuchaguliwa,” anasema.

“Lazima kuwepo na mazingira sahihi na muktadha sahihi wa kujadiliana na kukubaliana, lazima kuwepo na balance of power. CCM Zanzibar hawakukubali tu kwenda kwenye maridhiano kulikuwa na balance ambayo iliwalazimisha kukaa kwenye maridhiano, baada ya kushindwa uchaguzi,” anasema.

Zitto anasema maridhano wanayoyataka ni yule aliyechaguliwa na wananchi kupata ridhaa ya kuongoza kwa mujibu wa kura za wananchi na kwamba watakuwa tayari kwenda kwenye meza ya maridhiano na CCM kwa lengo la kuweka misingi ya uchaguzi huru na haki, kwamba yeyote atakayeshinda ataongoza wananchi.

“Katika maridhiano ya aina hiyo hata CCM wakishinda tuwape mkono na tutawaambia tukutane uchaguzi ujao, iwapo tukishinda sisi watupe mkono kwamba tumeshinda, ndio nchi za kistaarabu zinavyofanya,” anasema.

Suala la maridhiano si geni hapa nchini, kwani limeshawahi kutokea nchini mwaka 2010 kati ya CCM na CUF Zanzibar ambao waliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kujadiliana na kufikia muafaka wa kugawana madaraka, ili kuondoa siasa za chuki zilizotokana na machafuko ya mwaka 2005.

Kabla ya kufikiwa kwa mwafaka huo mwaka 2001 wafuasi 23 wa CUF waliuawa na wengine kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2000 katika mapambano na polisi.

Pia nchini Kenya, Machi 2018, liliundwa jopokazi la maridhiano maarufu kama BBI (Building Bridges Initiative), baada ya Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Raila Odinga walipoamua kuzika tofauti zao za kisiasa na kusalimiana hadharani.

Wamefikia hatua hiyo kwa lengo la kuunganisha taifa ambalo lilitumbukia katika uhasama baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017.

Zimbabwe nayo iliwahi kuingia mkataba wa maridhiano mwaka 1987 ambao ulimaliza mapigano kati ya kabila la Ndebele na Shona. Mkataba huo ulifanyika baada ya mapigano ya miaka kadhaa, huku maelfu ya Wandebele kuripitiwa kupoteza maisha.

Mwaka 2008 katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, mgombea wa upinzani, Morgan Tsvangirai kupitia MDC alionyesha ushindani mkali kwa Robert Mugabe wa Zanu –PF na kufanikiwa kupata kura asilimia 47 ya kura zilizopigwa dhidi ya asilimia 43 za Mugabe.

Tsvangirai alitaka atangazwe mshindi, lakini Tume ya Uchaguzi ikataka kura zipigwe tena katika duru la pili, hatua ambayo ilikataliwa na mgombea huyo akisema hautakuwa huru na wa haki.

Hali hiyo ilichangia kuibuka kwa vurugu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200. Viongozi wa jumuiya za kikanda waliingilia kati na kumtaka Mugabe kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa, Tsvangirai akawa waziri mkuu.

Maoni

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisema wanaunga mkono majadiliano na maridhiano kwa makundi yote ya kijamii kwa sababu ni moja ya misingi ya amani na maendeleo endelevu kwa jamii.

“Suala la maridhiano, upendo na mshikamano si tu ni la muhimu, bali ni la lazima kwa amani na maendeleo endelevu katika nchi yetu. Ninawaomba wanasiasa walitilie maanani,” alisema Askofu Shoo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga aliyesema maridhiano ni moja ya kanuni ya kuishi vizuri.

“Hata mkipigana na kila mtu kukasirika, mwafaka hupatikana kwa njia ya majadiliano na maridhiano...penye wengi hapaharibiki jambo,” alisema.

Akizungumzia hoja ya maridhiano, wakili wa kujitegemea, Frank Mushi alisema maridhiano yanapaswa yawe ya kitaifa na yalenge kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo yanayoikumba jamii

“Matatizo yetu mengi ya kisiasa na kiuchumi yanasababishwa na ulegevu wa taasisi zetu, sintofahamu wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni matokeo ya ulegevu wa taasisi na kukosekana uwajibikaji. Maridhiano yalenge kutatua kasoro hizo,” alisema Mushi.

Ni muhimu kuwapo kwa maridhiano, ili kunusuru nchi kuingia katika machafuko. Kutokana na umuhimu wa jambo hilo kuna kila sababu ya kutafutwa kwa ufumbuzi wa masuala yanayosabahisha mkwamo ili uchaguzi mkuu 2020 ufanyike kwa amani.

Hakuna haja ya kuendeleza uhasama, kwani vyama vyote vinajenga nyumba moja, hivyo si busara kugombania fito.

Chanzo: mwananchi.co.tz